Habari

WIZARA YA ARDHI YATOA ELIMU MATUMIZI BORA YA ARDHI MSOMERA LAIGWENANI WATAKA HATI MOJA WAKE WENGI

  • 27 Feb, 2024
WIZARA YA ARDHI YATOA ELIMU MATUMIZI BORA YA ARDHI MSOMERA LAIGWENANI WATAKA HATI MOJA WAKE WENGI

Timu ya wataalamu Wizara ya Ardhi ikiongozwa na Mthamini Mkuu wa Serikali Bi. Everyne Mugasha imefika eneo la Msomera Wilayani Handeni Mkoani Tanga kutoa elimu kwa jamii ya Kimasai kuhusu matumizi bora ya ardhi ili kujenga uelewa kwa jamii hiyo wa namna bora ya matumizi ya ardhi iliyopangwa kwa matumizi sahihi ya jamii hiyo.

 

Bi. Mugasha aliwaambia Viongozi na Wazee wa Kimila kuwa wanalo jukumu kubwa la kulinda miundombinu na maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya kilimo na malisho ili kudhibiti wavamizi ambao wanaweza kujitokeza na kuharibu malengo ya serikali yaliyopo.


Aidha Bi. Mugasha aliongeza kuwa Wizara inatoa kipaumbele  suala la ushirikishwaji wa wananchi katika mipango ya serikali ndio maana timu ya Wizara iko msomela kujionea namna gani wananchi wanashirikiana na serikali katika kuweka mipangp bora ya matumizi ya ardhi pamoja na uhifadhi wa mazingira katika eneo la msomera.


Katika hatua nyingine Mthamini huyo wa serikali alitaka kujua iwapo wananchi Msomera wamekuwa wakipatiwa hati za kimila kama hatua muhimu ya umilikishaji ardhi kwa wananchi hao ambao kimsingi wameonesha kupewa nyaraka hiyo muhimu kwa maendeleo yao.

 

Katika mazungumzo yao na timu hiyo Wazee hao kwa nyakati tofauti wameiomba serikali kufikiria upya suala la ugawaji ardhi zaidi kwa kaya za Kimasai kwani kwa mujibu wa mila zao wana ndoa za wanawake wengi jambo linalowapa changamoto kwani hati ya milki ya pamoja imendikwa mke mmoja.

 

''Jambo hili limeanza kujitokeza kama changamoto kwani baadhi ya wamasai wanaouliza kuwa baadae kama mwenye mji akitangulia mbele ya haki mali hii itakuwa ya nani kwani jina linaloandikwa kwenye hati ni la Bibi mmoja ili hali kabila la wamasai bado lina mila ya wanawake wengi.''Aliuliza Laigwenani wa Kimasai ambaye jina lake halikutambilika mara moja.

 

Timu ya wataalam kutoka Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imetoa elimu juu ya matumizi bora ya Ardhi kwa wananchi ambao wameamia eneo la Msomera Wilayani Handeni lengo likiwa ni kuahakikisha wananchi hao wanakuwa na ufahamu wa kutosha kuhusu mpango wa matumizi bora ya ardhi kwa manufaa yao ya baadae.
 

 

Aidha ardhi katika maeneo hayo imetengwa na kupimwa kwa ajili ya makazi, taasisi za umma kama vile zahanati, hospitali,shule  miundombinu ya maji, barabara pamoja na malisho ya Mifugo lengo likiwa ni kutoa huduma bora za kijamii kwa wakazi wapya wa eneo hilo walioamia toka ifadhi ya Taifa ya Ngorongoro..

 

Wizara ya Ardhi kupitia Tume yake ya Taifa ya Matumizi bora ya Ardhi imepima,kupanga na kumilikisha ardhi kwa wakazi wa zamani wa eneo hilo pamoja wahamiahaji hao ambapo kila kaya imepata ekari mbili na nusu kwa ajili ya makazi pamoja na ekari tano kwa matumizi ya kilimo na na ekari elfu 22 kwa ajili ya malisho.