Habari

WIZARA YA ARDHI YATEKELEZA ZAIDI YA ASILIMIA 86 YA MAPENDEKEZO YA CAG

  • 18 Aug, 2026
WIZARA YA ARDHI YATEKELEZA ZAIDI YA ASILIMIA 86 YA MAPENDEKEZO YA CAG

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi leo tarehe 17 Agosti 2026 imewasilisha taarifa ya utekelezaji wa maagizo na mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2024/2025 mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), huku ikieleza kuwa asilimia 86.36 ya mapendekezo yaliyotolewa tayari yametekelezwa.

 

Akijibu hoja za Kamati hiyo, Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhandisi Anthony Sanga, amesema kati ya mapendekezo 22 yaliyotolewa na CAG, mapendekezo 10 sawa na asilimia 45.45 yametekelezwa kikamilifu, huku mapendekezo tisa sawa na asilimia 40.91 yakiwa katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

 

Mhandisi Sanga amesema kwa ujumla, mapendekezo 19 kati ya 22, sawa na asilimia 86.36, yamefanyiwa kazi, hatua inayoonesha kuimarika kwa Wizara katika usimamizi wa fedha za umma, uwajibikaji na utekelezaji wa maelekezo ya Serikali na Bunge.

 

Aidha, amesema Wizara imeendelea kufanya vizuri katika utoaji wa huduma kwa wananchi, hususan katika eneo la umilikishaji wa ardhi, ambapo katika mwaka wa fedha 2025/2026 jumla ya Hatimiliki 123,968 zilitolewa pamoja na Hati ya Sehemu ya Jengo 957.

 

Ameeleza pia kuwa Wizara imenunua vifaa vyenye thamani ya takribani Shilingi bilioni 5.2, ikiwemo magari 80 kwa ajili ya kuimarisha utendaji wa shughuli za Wizara na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

 

Katika kuimarisha rasilimali watu, Mhandisi Sanga amesema Wizara imeongeza watumishi 469 katika mwaka wa fedha 2025/2026.

 

Kwa upande wa matumizi ya teknolojia, Wizara imeendelea kuimarisha matumizi ya Mfumo wa e-Ardhi pamoja na kuendesha Kliniki za Ardhi, zinazolenga kurahisisha upatikanaji wa huduma za ardhi na kuongeza kasi ya utoaji wa Hatimiliki kwa wananchi.

 

Hatua hizo zinaendana na jukumu la Wizara la kupanga, kupima na kurasimisha umiliki wa ardhi nchini, sambamba na kuboresha mifumo ya utoaji wa huduma na kuongeza uwazi na ufanisi katika sekta ya ardhi.

 

Pamoja na mafanikio hayo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Mhe. Devota Minja, ameitaka Wizara kuendelea kufuatilia na kukamilisha mapendekezo yaliyobaki, hususan katika maeneo ya kuimarisha mifumo ya TEHAMA na kuhakikisha usimikaji wa Mfumo wa e-Ardhi unakamilika katika mikoa yote 26 ndani ya miaka miwili.

 

Kikao hicho kimehudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bi. Lucy Kabyemera, Kamishna wa Ardhi, Bw. Nathaniel Mathew Nhonge, wajumbe wa Menejimenti ya Wizara pamoja na watumishi kutoka Wizara ya Fedha.