Habari

WIZARA YA ARDHI YATAKIWA KUSIMAMIA MAAZIMIO YA BUNGE

  • 21 Aug, 2024
WIZARA YA ARDHI YATAKIWA KUSIMAMIA MAAZIMIO YA BUNGE

Kamati ya Kudumu ya Ardhi Maliasili na Utalii imeitaka wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuendelea kusimamia maazimio ya Bunge ili kutoa huduma bora kwa Watanzania.

 

Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo na Mhe. Timotheo Mzava jijini Dodoma Agosti 20, 2024 wakati wa uwasilishaji taarifa za utendaji wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Utendaji wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya pamoja na utekelezaji wa Programu ya Kliniki za Ardhi nchini.

 

Mhe. Mzava amewasisitiza viongozi wa Wizara kuyafikia maeneo mengi nchini kupitia Programu ya Kliniki za Ardhi ambapo Makamishna wa Ardhi Wasaidizi wa mikoa wana wajibu wa kushirikiana na Wakuu wa Mikoa na Wilaya ili kuwahudumia Watanzania kwenye sekta ya Ardhi.

 

Akiwasilisha taarifa ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Mkurugenzi wa shirika hilo Bw. Hamad Abdallah amesema, kwa mwaka 2023/2024 shirika lake katika kipindi cha Julai 2023 hadi Juni 2024 limepata faida kabla ya kodi kiasi cha Sh. Bilioni 42.25 sawa na asilimia 147 na mtaji wake ulikuwa Sh. trilioni 5.16 ikilinganishwa na Sh. trilioni 5.04 Juni 2023.

 

Kwa upande wa Mabaraza, Mhe. Mzava

amesisitiza Wizara kuendelee kuboresha mifumo ya kusimamia Wenyeviti wa Mabaraza ili kupunguza malalamiko ya wananchi kwenye Mabaraza hayo katika maeneo mbalimbali nchini. 

 

Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya nchini yalianza kutoa huduma Oktoba, 2003 katika ngazi ya mikoa 23 iliyokuwepo kipindi hicho.

 

Ili kuwahudumia wananchi kwa karibu katika sekta ya Ardhi, Serikali imechukua hatua ya kusogeza huduma karibu na wananchi ambapo katika kipindi cha miaka 16 kuanzia mwaka 2004 hadi 2020, Wizara imeanzisha Mabaraza 32 katika ngazi ya Wilaya.

 

Mafanikio makubwa yameonekana katika kipindi cha miaka minne kuanzia mwaka 2020 hadi 2024 ambapo Mabaraza 55 yameanzishwa

na kufanya jumla ya Mabaraza 110 yanayotoa huduma kati ya Wilaya 139 zilizopo nchini.

 

Akielezea Programu ya Kliniki ya Ardhi, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe Deogratius Ndejembi amesema Wizara imefanikiwa kukusanya zaidi ya Sh. bilioni 3.8 ambapo hati miliki za ardhi 8,432 zimetolewa katika maeneo mbalimbali nchini.

 

Awali Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Ndejembi amesema Wizara hiyo itaendelea kufanyia kazi ushauri wa Kamati na wataendelea kusimamia maazimio ya Bunge na kuyatekeleza.

 

Kikao hicho cha Kamati kimehudhuriwa na Wajumbe wa Menejimenti ya Wizara hiyo wakiongozwa na Katibu Mkuu Mhandisi Anthony Sanga.