Habari
WIZARA YA ARDHI YASHIRIKI UZINDUZI WA WIKI YA SHERIA KWA MWAKA 2025
- 25 Jan, 2025

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia Kitengo cha Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya, imeshiriki rasmi uzinduzi wa Maadhimisho ya Wiki ya Sheria yaliyoanza leo, tarehe 25 Januari 2025, katika Viwanja vya Nyerere Square, jijini Dodoma.
Maadhimisho haya yanayoandaliwa kila mwaka na Mahakama ya Tanzania, mwaka huu yamebeba kauli mbiu isemayo: “Tanzania ya 2050: Nafasi ya Taasisi Zinazosimamia Haki katika Kufikia Malengo Makuu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo.”
Mgeni rasmi katika uzinduzi wa maadhimisho haya ni Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, ambaye amesisitiza umuhimu wa taasisi za haki katika kuchochea maendeleo endelevu ya taifa.
Wizara ya Ardhi imeweka mkakati wa kutumia maadhimisho haya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu masuala mbalimbali ya ardhi, ikiwa ni pamoja na haki za umiliki wa ardhi, utatuzi wa migogoro ya ardhi, na huduma zinazotolewa na mabaraza ya ardhi. Huduma hizo zitapatikana katika banda la Wizara wakati wote wa maadhimisho hayo.