Habari

WIZARA YA ARDHI YASHIRIKI MAFUNZO YA MIFUMO YA USIMAMIZI UPIMAJI NA MILKI NAIROBI

  • 17 Sep, 2026
WIZARA YA ARDHI YASHIRIKI MAFUNZO YA MIFUMO YA USIMAMIZI UPIMAJI NA MILKI NAIROBI

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi inashiriki mafunzo ya wiki moja kuhusu mifumo ya usimamizi wa upimaji na milki za ardhi, yanayofanyika jijini Nairobi, Kenya.

 

Mafunzo hayo yameanza tarehe 14 Septemba na yanatarajiwa kuhitimishwa tarehe 18 Septemba 2026, yakishirikisha wawakilishi kutoka nchi 20 wanachama wa Regional Centre for Mapping of Resources for Development (RCMRD).

 

Lengo la mafunzo hayo ni kujenga uwezo, kubadilishana uzoefu na kujifunza mbinu mbalimbali za matumizi ya mifumo ya kidijiti katika usimamizi wa taarifa za ardhi na utoaji wa huduma za upimaji na milki.

 

Akizungumza kuhusu ushiriki wa Wizara katika mafunzo hayo, Afisa Ramani Mwandamizi kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bw. Masoud Waziri Self, amesema mafunzo hayo ni fursa muhimu ya kujenga uwezo wa wataalamu na kupata uzoefu kutoka nchi jirani na zile za ukanda wa Afrika katika matumizi ya mifumo ya kidijiti kwa ajili ya kuboresha huduma za ardhi.

 

Ameeleza kuwa, mafunzo hayo yamejikita katika matumizi ya mifumo ya kidijiti katika usanifu, uandaaji na usimamizi wa kanzidata za taarifa za viwanja, pamoja na namna ya kusimamia taarifa hizo kwa ufanisi ili kurahisisha upatikanaji na matumizi ya taarifa za ardhi.

 

“Mafunzo haya yanatupa fursa ya kujifunza kutoka nchi nyingine wanachama wa RCMRD kuhusu matumizi ya mifumo katika utoaji wa huduma za ardhi, hususan katika eneo la upimaji na usimamizi wa milki,” amesema Bw. Masoud.

 

Aidha, amesema mafunzo hayo yanatoa uelewa kuhusu namna ya kuunganisha mifumo yenye taarifa mbalimbali za viwanja, hatua inayoweza kusaidia kuongeza ufanisi katika usimamizi wa taarifa za ardhi na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

 

Mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za nchi wanachama wa RCMRD kuimarisha uwezo wa wataalamu katika matumizi ya teknolojia na mifumo ya kisasa katika usimamizi wa rasilimali ardhi, huku yakitoa fursa kwa washiriki kubadilishana uzoefu, mbinu na maarifa yatakayosaidia kuboresha huduma katika nchi zao.