Habari
WIZARA YA ARDHI YALENGA KUWA KINARA WA UANDAAJI RAMANI AFRIKA
- 04 Nov, 2026
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi inalenga kuijengea uwezo endelevu Tanzania kuandaa na kuhuisha ramani za msingi, ili kujitegemea katika huduma hizo na hatimaye kuzitoa kwa nchi nyingine za Afrika.
Hayo yamesemwa leo Novemba 3, 2026 jijini Dodoma na Kamishna wa Ardhi, Bw. Nathaniel Methew, kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bi. Lucy Kabyemera, wakati wa mafunzo kwa Timu ya Utekelezaji Mradi (PIT) wa Kuimarisha Miundombinu ya Upimaji na Ramani (NLDI).
Bw. Nhonge amesema, kuijengea uwezo huo Tanzania hakulengi kupata ramani pekee, bali pia kuwajenga uwezo wataalamu wa ndani ili Tanzania isiendelee kutegemea wataalamu kutoka nje.
"Niitake timu ya PIT kuandaa mikakati pia ya kuwajengea uwezo wataalamu ndani na nje ya nchi sambamba na kuwaelimisha kuhusu matumizi ya teknolojia za kisasa, ikiwemo Akili Unde (AI) katika ukusanyaji wa taarifa za ramani na Blockchain katika kuimarisha usalama wa miamala ya umiliki wa ardhi". Amesema
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha wataalamu wanaopata mafunzo wanahamisha ujuzi huo kwa wengine, na kuelekeza mapendekezo ya utekelezaji wa mikakati hiyo yawasilishwe ndani ya miezi miwili.
Kwa mujibu wa Bw. Nhonge, mradi huo unahusisha upatikanaji wa vifaa na mifumo ya kisasa, ikiwemo ndege za kupiga picha za anga, vituo vya upimaji vya kielektroniki (CORS) na Miundombinu ya Taifa ya Taarifa za Kijiografia (NSDI), vitakavyosaidia kuboresha uandaaji wa ramani na matumizi ya taarifa za kijiografia nchini.
Kwa upande wao, wajumbe wa Timu ya Utekelezaji Mradi (PIT) wamesema mafunzo hayo yamewaongezea uelewa na ujuzi wa kutekeleza majukumu yao kwa weledi na ufanisi, kwa kuzingatia maelekezo yaliyotolewa.
Mradi wa NLDI unatekelezwa kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 65, kwa ufadhili wa Serikali ya Jamhuri ya Korea, ukiwa na lengo la kuimarisha uwezo wa Tanzania katika upimaji, uandaaji wa ramani na usimamizi wa taarifa za kijiografia.