Habari

WIZARA YA ARDHI YAKUSANYA BILIONI 191.90 ZA KODI YA PANGO LA ARDHI

  • 04 Jun, 2026
WIZARA YA ARDHI YAKUSANYA BILIONI 191.90 ZA KODI YA PANGO LA ARDHI

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imekusanya kiasi cha shilingi bilioni 191.90 hadi kufikia Mei 15, 2026.

 

Hayo yamebainishwa Mei 28, 2026 na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo wakati akiwasilisha makadirio ya bajeti ya Wizara yake kwa mwaka wa fedha 2026/207 Bungeni jijini Dodoma.

 

Amesema, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2026/27, Wizara yake imepanga kukusanya shilingi bilioni 300 kutokana na Kodi ya Pango la Ardhi, ada na tozo mbalimbali zinazohusiana na sekta ya ardhi.

 

Kwa mujibu wa Mhe. Dkt. Akwilapo, lengo la ukusanyaji kiasi hicho cha fedha litafikiwa kwa kutekeleza mikakati mbalimbali.

 

Ameitaja baadhi ya mikakati hiyo kuwa ni kuendelea kusambaza miundombinu na mifumo ya TEHAMA katika Ofisi za Ardhi za Mikoa na Halmashauri ili kurahisisha utoaji wa huduma za ardhi; kuendelea kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu -TAMISEMI kufuatilia halmashauri ambazo hazijakamilisha utekelezaji wa miradi ya KKK na kuchukua hatua za kisheria kwa wadaiwa sugu ikiwemo kuwafikisha mahakamani. 

 

Aidha, Amesema, Wizara ya Ardhi kwa kushirikiana na mamlaka nyingine inaendelea kutafuta njia bora ya ukusanyaji wa kodi ya pango la ardhi kupitia huduma mbalimbali zinazotolewa na taasisi hizo. 

 

Ametoa rai kwa wamiliki wote wa ardhi kuhakikisha wanatekeleza wajibu wao wa msingi wa kulipa kodi ya pango la ardhi kwa wakati ili kuepuka kuchukuliwa hatua za kisheria, ikiwemo kufutiwa umiliki.