Habari

WIZARA YA ARDHI YAKAMILISHA ZOEZI LA KUONESHA MIPAKA YA VIWANJA ENEO LA UWANJA WA NDEGE WA SANZALE, BAGAMOYO

  • 26 Oct, 2026
WIZARA YA ARDHI YAKAMILISHA ZOEZI LA KUONESHA MIPAKA YA VIWANJA ENEO LA UWANJA WA NDEGE WA SANZALE, BAGAMOYO

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imekamilisha zoezi la kuonesha mipaka ya maeneo ya wananchi yaliyopo ndani ya eneo la Uwanja wa Ndege wa Sanzale, wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani, kufuatia ombi la wananchi hao kutaka kufahamu na kupata ufafanuzi wa mipaka ya maeneo yao.

 

Zoezi hilo limefanyika leo, tarehe 22 Oktoba 2026, likijumuisha uoneshaji mipaka ya Kiwanja Na. 1 Sanzale, hatua iliyolenga kuwawezesha wananchi kutambua maeneo yanayohusika na kupata ufafanuzi wa mipaka yake.

 

Akisimamia utekelezaji wa zoezi hilo, Naibu Kamishna wa Ardhi Bw. Hussein Sadick, amesisitiza umuhimu wa kushughulikia masuala ya ardhi kwa weledi, haki na kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa, huku haki na maslahi ya wananchi yakizingatiwa.

 

Kukamilika kwa zoezi hilo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, aliyoyatoa kufuatia wananchi kuwasilisha changamoto zao kuhusu mipaka ya maeneo hayo wakati wa ziara yake ya kikazi wilayani Bagamoyo.

 

Wananchi hao waliiomba Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuwasaidia kupata ufafanuzi wa mipaka ya maeneo yao.

 

Katika hatua nyingine, wataalamu wa Wizara hiyo wanaendelea kutoa huduma kupitia Kliniki Maalum ya Ardhi wilayani Bagamoyo, iliyoanza tarehe 19 Oktoba 2026 na inayotarajiwa kuhitimishwa tarehe 23 Oktoba 2026.

 

Kliniki hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Waziri Mkuu, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, aliyeelekeza Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji na Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA), kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kushughulikia changamoto za ardhi katika maeneo yanayohitajika kwa uwekezaji ndani ya Eneo Maalumu la Kiuchumi.

 

Kupitia kliniki hiyo, wananchi wanapata fursa ya kuwasilisha kero zao, kupata ufafanuzi kuhusu masuala ya umiliki na mipaka ya ardhi, pamoja na kupata huduma za kitaalamu kwa changamoto zinazohitaji uingiliaji wa wataalamu wa sekta ya ardhi.