Habari

WIZARA YA ARDHI YAIMARISHA UWEZO WA WATAALAM WAKE KATIKA MATUMIZI YA ARCGIS PRO

  • 31 Jul, 2026
WIZARA YA ARDHI YAIMARISHA UWEZO WA WATAALAM WAKE KATIKA MATUMIZI YA ARCGIS PRO

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeanza mafunzo ya matumizi ya maunzi laini ya ArcGIS Pro yanayolenga kuwajengea uwezo wataalamu wa Idara ya Upimaji na Ramani ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za ramani na usimamizi wa taarifa za kijiografia.

 

Mafunzo hayo pia yatawawezesha washiriki kutumia ArcGIS Pro katika uchakataji na uchambuzi wa picha za angani, ukusanyaji wa taarifa za upimaji pamoja na uandaaji wa ramani zenye ubora na usahihi zaidi.

 

Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani, Julai 27, 2026, Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Ramani, Bw. Joseph Ikorogo, amewataka washiriki kuyatumia vyema mafunzo hayo kwa kujifunza kwa bidii ili kujipatia maarifa na ujuzi utakaowawezesha kuboresha utendaji wao wa kazi na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma

 

Bw. Ikorogo amesema, Wizara ya Ardhi inatarajia kuona matokeo chanya yatakayotokana na mafunzo hayo aliyoyaeleza kuwa yanaongeza ufanisi wa kazi za kiramani na kuimarisha uwezo wa Wizara katika kupanua wigo wa huduma zake kwa kutumia teknolojia za kisasa za mifumo ya taarifa za kijiografia (GIS).

 

Naye Mhandisi wa Mifumo ya Taarifa za Kijiografia (GIS) wa Esri Eastern Africa Bi Latimar Mkohe amesema, mafunzo hayo ni sehemu ya mpango wa kuwawezesha wataalamu wa sekta ya Ardhi kutumia kikamilifu teknolojia za kisasa za mifumo ya taarifa za kijiografia (GIS) katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

 

Bi. Mkohe ameongeza kuwa, washiriki pia watapatiwa ujuzi wa kutumia mfumo wa ArcGIS Enterprise katika kuhifadhi, kusimamia na kushirikisha taarifa za kijiografia kwa ufanisi, hatua ambayo itasaidia kuimarisha utendaji wa Wizara na kuongeza ubora wa huduma zinazotolewa kwa wananchi kupitia matumizi ya teknolojia za kisasa za GIS.

 

Mafunzo hayo ya siku kumi yanawahusisha watumishi wa Idara ya Upimaji na Ramani kutoka Makao Makuu ya Wizara, Dodoma, na yanaendeshwa na wakufunzi kutoka Esri Eastern Africa.