Habari

WIZARA YA ARDHI YAHAKIKI VIWANJA NA MASHAMBA ZAIDI YA 2,305 KATIKA ENEO LA MAKINYUMBI, HALE TANGA

  • 18 Nov, 2026
WIZARA YA ARDHI YAHAKIKI VIWANJA NA MASHAMBA ZAIDI YA 2,305 KATIKA ENEO LA MAKINYUMBI, HALE TANGA

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeendelea kutekeleza maelekezo ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa kufanya zoezi la utambuzi na uhakiki wa viwanja na mashamba zaidi ya 2, 305 katika eneo la Makinyumbi lililopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga huku taarifa za wamiliki 2,228 zikikusanywa.

 

Akizungumzia maendeleo ya zoezi hilo tarehe 17 Novemba 2026 wilayani Korogwe mkoani Tanga, Mpima Ardhi kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeo ya Makazi Bw. Johnson Kashaija, amesema utekelezaji wa zoezi hilo unaendelea vizuri, huku wataalamu wakiendelea kufanya utambuzi na uhakiki wa maeneo yaliyopo ndani ya shamba la Makinyumbi.

 

Amesema, zoezi hilo linatekelezwa kufuatia maazimio ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii iliyoagiza kufanyika uhakiki wa mashamba na makazi yaliyopo eneo hilo lenye ukubwa wa hekta 3,200, ili kubaini ukubwa halisi wa maeneo, hali ya umiliki na shughuli mbalimbali zinazofanyika, hatua itakayosaidia maandalizi ya uendelezaji wa eneo hilo.

 

Kwa upande wake, Afisa Ardhi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga, Bw. George Mathias Gamba, amesema Halmashauri hiyo kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi inatekeleza maelekezo ya Kamati hiyo kwa kuanza haraka zoezi la utambuzi na uhakiki wa eneo la Makinyumbi.

 

Ameeleza kuwa, zoezi hilo pia linalenga kuwatambua wananchi waliopo katika eneo hilo, kubaini hali ya umiliki wa maeneo wanayoyatumia na kuweka msingi wa kushughulikia masuala ya umilikishaji kwa mujibu wa sheria na taratibu za ardhi nchini.

 

Mmoja wa wataalamu wanaoshiriki zoezi hilo, Mpima Ardhi kutoka Halmashauri ya Mji wa Korogwe, Bi. Loveness Michael Angalo amesema wataalamu wamejipanga kikamilifu na wanatumia vifaa vya kisasa vya upimaji ili kuhakikisha utambuzi na uhakiki unafanyika kwa usahihi na ufanisi.

 

Aidha, amewahimiza wananchi wenye maeneo katika eneo la Makinyumbi kujitokeza kwa wingi kushiriki zoezi hilo na kutoa taarifa sahihi zinazohitajika ili kurahisisha uhakiki wa maeneo na taarifa za umiliki.

 

Zoezi hilo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuimarisha usimamizi wa ardhi, kuweka kumbukumbu sahihi za umiliki na kuhakikisha matumizi na uendelezaji wa ardhi yanafanyika kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa.