Habari
WIZARA YA ARDHI YAENDELEA KUBORESHA MIFUMO YA UTOAJI WA HUDUMA BORA KWA WANANCHI
- 30 Oct, 2026
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeendelea kuboresha upatikanaji na utoaji wa huduma kwa wananchi kupitia mifumo ya kidijiti inayorahisisha umilikishaji wa ardhi na kuhakikisha wananchi wanapata hati za ardhi kwa urahisi na kwa wakati, bila usumbufu.
Hayo yamebainishwa leo, Oktoba 29, 2026, na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhandisi Anthony Sanga, wakati akizungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari ofisini kwake kuhusu mipango na utekelezaji wa majukumu ya Wizara.
Mhandisi Sanga amesema Wizara imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi, ikiwemo kuanzisha na kuimarisha mfumo wa kidijiti wa e-Ardhi, ambao umeenea katika mikoa 17 nchini.
Amesema mfumo huo umesaidia kupunguza usumbufu ambao wananchi walikuwa wakikumbana nao katika mchakato wa kupata hati za viwanja vyao.
“Tumendelea kuboresha suala zima la umilikishaji wa ardhi, hususan kuhakikisha wananchi wanapata hati zao. Pia, tumeboresha mfumo wa e-Ardhi ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi,” amesema Mhandisi Sanga.
Aidha, Mhandisi Sanga amesema Serikali chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeendelea kuimarisha sekta ya ardhi kwa kuajiri watendaji zaidi pia maboresho ya miundombinu ya majengo ya Wizara pamoja na ongezeko la vitendea kazi, ikiwemo magari, yamechangia kuboresha mazingira ya utendaji kazi na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Kwa upande wake, Kamishna wa Ardhi wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bw. Nathaniel Mathew Nhonge, amesema majukumu makuu ya Wizara ni kupanga ardhi, kupima ardhi na kumilikisha ardhi kwa wananchi.
Ameeleza kuwa, pamoja na majukumu hayo, Wizara pia inasimamia shughuli za uthamini wa mali kwa ajili ya ulipaji wa fidia kwa wananchi, hususan katika maeneo yanayotwaliwa na Serikali kwa matumizi mbalimbali ya umma.