Habari

WIZARA YA ARDHI YAANZA KUTEKELEZA AGIZO LA WAZIRI MKUU BAGAMOYO

  • 20 Oct, 2026
WIZARA YA ARDHI YAANZA KUTEKELEZA AGIZO LA WAZIRI MKUU BAGAMOYO

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeanza kutekeleza agizo la Waziri Mkuu, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, la kushughulikia changamoto za ardhi kwenye maeneo yanayohitajika kwa uwekezaji katika Eneo Maalumu la Kiuchumi Bagamoyo mkoani Pwani kwa kuendesha Kliniki Maalum ya Ardhi wilayani humo.

 

Waziri Mkuu alitoa agizo hilo Oktoba 16, 2026, wakati akikagua maendeleo ya Ujenzi wa Kongani ya Viwanda ya Kampuni ya Hongwang Tanzania (HWTZ SEZ Limited), wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani.

 

Akizungumza katika Viwanja vya Shule ya Msingi Majengo, Bagamoyo Oktoba 19, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo, amesema wizara yake imeanza kutekeleza maagizo hayo ya Waziri Mkuu kwa kuendesha Kliniki Maalum ya Ardhi inayolenga kuwasaidia wananchi kupata ufumbuzi wa changamoto za ardhi kwa urahisi.

 

Amesema Kliniki hiyo ya Ardhi itafanyika kwa kipindi cha wiki moja kuanzia Oktoba 19, 2026. Hata hivyo ameeleza kuwa muda wa kliniki hiyo unaweza kuongezwa kulingana na changamoto mbalimbali za ardhi zitakazojitokeza.

 

Ametaja changamoto kubwa kwenye migogoro ya ardhi wilayani Bagamoyo mkoa wa Pwani kuwa ni uvamizi wa maeneo ambayo tayari yana wamiliki halali.

 

"Nitoe wito kwa wananchi wa Bagamoyo na Tanzania kwa ujumla kuheshimu haki za umiliki wa ardhi na kufanya uhakiki wa kina kabla ya kununua viwanja au mashamba kwa mamlaka husika ili kuepuka migogoro". Amesema

 

Amesema, hatua ya kufanya uhakiki kabla ya kununua eneo ni muhimu katika kuzuia migogoro ya ardhi inayoweza kusababishwa na ununuzi wa maeneo yenye matatizo ya umiliki.

 

Ameongeza kuwa, maeneo yenye hukumu za mahakama yanapaswa pia kushughulikiwa kwa kuzingatia maamuzi yaliyotolewa na mahakama, huku akieleza kuwa Wizara yake itaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kufuata taratibu za kisheria katika masuala ya ardhi. 

 

Kliniki hiyo Maalum ya Ardhi katika eneo la Bagamoyo mkoa wa Pwani inaongozwa na Kamishna wa Ardhi, Bw. Nathaniel Nhonge, Naibu Kamishna wa Ardhi, Hussein Sadick, pamoja na wataalamu wengine wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi.