Habari
WIZARA NA TAASISI ZA UMMA WEKENI PROGRAM ZA MAZOEZI YA WATUMISHI – BALOZI DKT. KUSILUKA
- 13 Aug, 2024
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeshiriki uzinduzi wa michuano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali Tanzania (SHIMIWI) ambapo taasisi hizo zimehimizwa kuandaa programu za mazoezi na michezo kuanzia sasa.
Ili kufanikisha azma hiyo, Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi Dkt. Moses Kusiluka amezitaka Wizara na Taasisi za Umma kuhakikisha wanatenga bajeti na kuweka programu ya michezo katika maeneo yao ya kazi kwani michezo ni muhimu kama shughuli zingine zozote.
Balozi Dkt. Kusiluka ametoa rai hiyo Agosti 10, 2024 jijini Dodoma, katika bonanza la uzinduzi wa michuanio ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali Tanzania (SHIMIWI), ,ambapo amesema siku moja haitoshi kwa michezo hivyo ni vema kila Idara iandae programu za mazoezi na michezo na ataanza kuzifuatilia kuanzia sasa.
"Mimi mwenyewe nafanya mazoezi na ofisini pale tuna eneo maalumu la kufanyia mazoezi hivyo nizitake Wizara na Idara za Serikali kuwa na Programu za mazoezi, mtambue kila mtu kulingana na umri wake anapaswa kufanya mazoezi tena unapokuwa na umri mkubwa unahitaji mazoezi zaidi, yapo mazoezi ya watu wenye afya na hata wagonjwa wanamazoezi yao, ukiangalia sasa kuna michezo ya Olimpiki inayoendelea kuna mchezo wa kutembea, hivyo hata kutembea ni mazoezi" amesema Balozi Dkt. Kusiluka
Amewataka viongozi wote kuanzia Makatibu Wakuu kuhakikisha wanampatia taarifa ya namna gani wameandaa bajeti kwa ajili ya michezo na michuano mbalimbali, kutokuwa na bajeti kisiwe kikwazo kwa watumishi kutoshiriki katika michezo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa SHIMIWI, Daniel Mwalusamba amesema mashindano ya SHIMIWI kwa mwaka 2024 yatafanyika mkoani Morogoro kuanzia Septemba 18 hadi Oktoba 5, amewaomba waajiri kuwaruhusu mapema watumishi wao ambao ni wanamichezo kushiriki michezo hiyo ili ianze kwa kwa wakati bila kuathiri ratiba za mechi zitakazokuwa tayari zimepangwa kwenye ratiba.
"Kumbukumbu tulizonazo baadhi ya timu zimekuwa zikichelewa sana kufika katika kituo cha mashindano hali inayopelekea kuvurugika kwa ratiba hivyo tuwaombe waajiri kuwaruhusu mapema wanamichezo kuja kushiriki mashindano ya SHIMIWI kwa wakati ili kuepukana na kupanguapangua ratiba mara kwa mara," amesisitiza Mwalusamba.
Lengo Kuu la mashindano ya SHIMIWI ni kuhakikisha watumishi wa umma wanakuwa na afya njema, ili waweze kutoa mchango wa ujenzi endelevu wa taifa hivyo michezo ni eneo salama la kutunza afya za Watumishi, kwa ajili ya maendeleo ya taifa endelevu.