Habari

WENGI WAJITOKEZA KUPATA HUDUMA KATIKA KLINIK YA ARDHI MAFINGA

  • 16 Sep, 2025
WENGI WAJITOKEZA KUPATA HUDUMA KATIKA KLINIK YA ARDHI MAFINGA

Zaidi ya wananchi 139 wamejitokeza katika siku ya kwanza ya Kliniki ya Ardhi inayoendelea katika kata ya Upendo Hamashauri ya Mji wa Mafinga mkoani Iringa.

Kliniki hiyo ya Ardhi itakayofanyika kwa siku sita imeanza tarehe 15 Septemba 2025 na inatarajiwa kukamilika siku ya Ijumaa tarehe 19 Septemba 2025.

Akizungumza katika kliniki hiyo kwa niaba ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi wa mkoa wa Iringa Bi. Rehema Kilonzi, Afisa Ardhi Mteule wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga Geofrey Kabuje amesema, muitikio wa wananchi wanaohitaji huduma za sekta ya ardhi kwenye klinik hiyo umekuwa mkubwa kutokana na wananchi kuhamasika.

''Katika siku ya kwanza ya Kliniki ya Ardhi katika kata hii ya Upendo muitikio wa wananchi ni mkubwa sana ambapo takriban wananchi 139 wamejitokeza kupata huduma'' amesema

Amezitaja huduma zinazotolewa kupitia kliniki hiyo kuwa ni pamoja na utayarishaji hati milki za ardhi, kupokea, kusikiliza na kutatua changamoto za ardhi, kutoa ushauri wa masuala mbalimbali ya ardhi, kukadiria kodi ya pango la ardhi sambamba na kutoa elimu juu ya sheria ya ardhi.

Kwa mujibu wa Afisa Ardhi Mteule wa halmashauri ya Mji wa Mafinga, zoezi la Kliniki ya ardhi katika kata ya Upendo linafanyika kuanzia saa 2:30 asubuhi hadi saa 10:00 jioni  katika ofisi ya kata ya Upendo lengo likiwa kuhakikisha changamoto za ardhi zinatatuliwa na wananchi wanapata huduma za ardhi kwa wakati.