Habari

WAZIRI SILAA: FANYENI KAZI KWA UADILIFU 

  • 29 May, 2024
WAZIRI SILAA: FANYENI KAZI KWA UADILIFU 

Makamishna wa Ardhi Wasaidizi nchini wametakiwa kufanya kazi kwa uadilifu wakitabua kila maamuzi wanayoyafanya yanaishi na wawe na uwezo wa kuelezea wamefikiaje maamuzi hayo ili watu wengine wakipitia watambue kweli kazi ya kuridhisha imefanyika.

 

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa wakati akiongea na Makamishna hao kutoka mikoa yote Tanzania Bara jijini Dodoma Mei 28, 2024 mara baada ya bajeti ya Wizara hiyo   kupitishwa na Bunge Mei 27, 2024.

 

"Mikoa yote niliyopita, naridhishwa sana na utendaji wenu wa kazi. Nilazima huko mikoani msimamie suala la ardhi, nawapa mfano wa Kamishna wa Mwanza anafanya kazi vizuri, anashauri na taarifa yake kwenye kumbukumbu, government moves on paper. Ukiona Waziri yeyote anakuagiza jambon a unaona limekaa kushoto mwandikie dokezo kwa Kamishna wa Ardhi" amesema Waziri Silaa.

 

Amesema ni lazima uwepo utaratibu mzuri wa kufanyakazi kama wizara kwa kuwapa watumishi mafunzo ya kufanyakazi kikamilifu ili kuwahudumia wananachi na kusisitiza kuwa kuna kazi kubwa ya kujipanga kufanyakazi kama taasisi.

 

Aidha, Waziri Silaa amesema Kliniki za Ardhi zitaendelea katika mikoa yote ili kuendelea kutatua na kumaliza migorogoro ya ardhi katika maeneo mbalimbali nchini.

 

Akimkaribisha Waziri kuongea na Makamishna hao, Katibu Mkuu Wizara hiyo Mhandisi Anthony Sanga amewakumbusha kuhusu misingi sita ya kufanyakazi aliyotoa Mhe. Waziri akijibu hoja za Wabunge wakati kupitisha bajeti ya wizara hiyo kuwa ili watendaji wa wizara wazingatie kwenye utendaji wao wa kazi.

 

Misingi hiyo ni uharaka wa jambo wakati unafanyakazi ya umma kwa sababu wananchi wanaohudumiwa wanahitaji kwenda kufanya shughuli zao, msingi wa pili ni kujali na kutoa huduma ni lazima kuwajali watanzania na kuwahudumia kwa upendo, msingi wa tatu ni nidhamu ya kujali muda, kujali na kuheshimu watu, msingi wa nne ni lazima kuwasikiliza na kuwaelewa, ukimsikiliza mwananchi ni lazima umsikilize kwa makini ili umwelewe na kumtatulia tatizo lake, msingi wa tano ni lazima kuwa na majawabu ya matatizo ya watanzania na msingi wa sita ni lazima kufanyakazi kwa uadilifu.