Habari

WAZIRI NDEJEMBI: FANYENI KAZI KWA WELEDI MKITANGULIZA MASLAHI YA TAIFA 

  • 23 Sep, 2024
WAZIRI NDEJEMBI: FANYENI KAZI KWA WELEDI MKITANGULIZA MASLAHI YA TAIFA 

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Deogratius Ndejembi amewataka Maafisa Ardhi kutouza holela ardhi hali ambayo imekuwa chanzo cha migogoro ya ardhi sehemu mbalimbali nchini.

 

Mhe. Ndejembi ametoa agizo hilo wakati akizungumza na Maafisa Ardhi wa Mkoa wa Ruvuma ambapo amewataka kufanya kazi kwa weledi huku wakisimamia taaluma zao kwa ajili ya maslahi mapana ya Taifa.

 

“Tuna kazi kubwa ya kuhakikisha tunapima Nchi yetu, tunaipanga na kusubiri kumilikisha. Tuna jukumu kubwa la kuhakikisha tunaangalia mbele kabla ya migogoro kutokea, ndio maana Serikali inataka mfanye kazi kwa weledi kwa kuweka maslahi ya Taifa letu mbele.

 

Hatutosita kumchukulia hatua kali mtu yeyote ambaye atashindwa kutumia taaluma yake vizuri kwa kuruhusu uuzaji holela wa ardhi ambao umekua ukisababisha migogoro mingi ya ardhi” amesema Mhe. Ndejembi.

 

Aidha, amewataka Maafisa Ardhi hao kulifanya zoezi la kuwasikiliza wananchi kuwa endelevu na kusisitiza wananchi kupewa huduma stahiki kwa lugha nzuri yenye staha.