Habari

Waziri Ndejembi awataka wadaiwa pango la ardhi kulipa

  • 06 Mar, 2025
Waziri Ndejembi awataka wadaiwa pango la ardhi kulipa

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Deogratius Ndejembi amewataka wadau wa sekta ya ardhi nchini ambao wanadaiwa pango la ardhi kulipa deni hilo kabla ya mwaka wa fedha 2024/25 kumalizika.

Mhe. Ndejembi ametoa agizo hilo Machi 05, 2025 wakati akizungumza katika kikao kazi cha Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na wadau wa sekta ya ardhi kilichofanyika jijini Dar wa Salaam.

Aidha amechukua ombi la wadau hao la kutolewa kwa riba na kuahidi kulipeleka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan kumuomba kutoa riba na tozo zilizokua kwenye kodi ya pango la ardhi kwa wadaiwa na kulipa deni halisi kama alivyofanya mwaka 2023/24.

Amesema Serikali itahakikisha kunakua na mfumo rahisi wa kuweza kufanya mmiliki wa ardhi kulipa kodi yake kirahisi.

“ Vilevile niwatake wale wote wenye mashauri kwenye Halmashauri na Mahakama ambayo hayajapatiwa ufumbuzi waandike barua kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ajili ya kuelezea wameshindwa kulipa kwa sababu ya kutopata uhakika wa umiliki wa ardhi hadi mashauri yao yatakapokua yamefika mwisho,” Amesema Mhe. Ndejembi.

Awali akizungumza katika kikao hicho, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Mkazi, Lucy Kabyemera amesema jumla ya wamiliki wa ardhi 636 wamehakikiwa na kubainika kuwa na deni la pango la ardhi la thamani ya Sh Bilioni 44 zikiwemo Kampuni 18, Taasisi za Umma na Binafsi pamoja na watu binafsi.