Habari

Waziri Ndejembi Aingilia Mgogoro wa Ardhi kati ya Wananchi wa Lunyanywi na KKKT Njombe

  • 03 Apr, 2025
Waziri Ndejembi Aingilia Mgogoro wa Ardhi kati ya Wananchi wa Lunyanywi na KKKT Njombe

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Deogratius Ndejembi leo Aprili 3, 2025, amefanya ziara ya siku moja mkoani Njombe kwa lengo la kusikiliza na kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa muda mrefu wa ardhi kati ya wananchi wa eneo la Lunyanywi na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Njombe (KKKT).

Katika ziara hiyo, Mhe Ndejembi alisikiliza pande zote wakiwemo viongozi wa kanisa wakiongozwa na Askofu wa Dayosisi ya Njombe, Dkt. George Fihavango, Viongozi wa Mkoa na Wilaya, Kata na Kijiji.

Baada ya kupitia nyaraka za umiliki wa ardhi na kujiridhisha na uhalali wa eneo husika, Mhe. Ndejembi amewataka wananchi wote waliovamia eneo la Kanisa kuacha mara moja na kusubiri maamuzi rasmi ya Serikali. 

"Natoa katazo rasmi, kuanzia sasa mtu yeyote haruhusiwi kuendeleza ujenzi wowote katika eneo hili na yeyote atakayekaidi agizo hili hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

Lakini pia nimtake Mhe Mkuu wa Wilaya kutumia vyombo vya Ulinzi na Usalama kwa maana ya TAKUKURU kuhakikisha wanapitia nyaraka zote za wale waliouziwa na watu ambao siyo kanisa na kama kuna watumishi wa Serikali waliohusika kusaini nyaraka nao wachukuliwe hatua za kisheria,”Amesema Mhe. Ndejembi.