Habari
WAZIRI NDEJEMBI AAGIZA MJANE KUKABIDHIWA NYUMBA YAKE NDANI YA SIKU 14
- 23 Jul, 2025

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Deogratius Ndejembi amemuelekeza Kamishna wa Ardhi Mkoa wa Dar es Salaam kushirikiana na Vyombo vya Ulinzi na Usalama kuhakikisha ndani ya siku 14 Mjane wa Marehemu Fadhil Hussein Omari anakabidhiwa Nyumba yake iliyokua imepangishwa kwa Kwa Kampuni ya Barretto Hauliers mali ya Richard Baretto.
Mhe. Ndejembi ametoa agizo hilo mara baada ya kufika katika Nyumba hiyo iliyopo Kurasini, Dar es Salaam kufuatia kupokea malalamiko kutoka kwa Bi. Halima Omari ambaye alilalamika mpangaji wake, Kampuni ya Barretto Hauliers kukiuka mkataba wa upangishwaji wa nyumba hiyo tokea kufariki kwa Mumewe, Bw. Fadhil Omari.
“ Mama huyu Mjane ndiyo msimamizi halali wa mirathi hii ya Mume wake, na kwa muda mrefu Kampuni hii ya Barretto Hauliers imekua ikisumbua kulipa kodi kwa mujibu wa mkataba ambao mliingia wakati ukipangishiwa nyumba hii.
Sasa ninatoa siku 14 kwa mmiliki wa Kampuni hii uwe umeondoa mali zako na umkabidhi Mama huyu nyumba yake. Ndani ya muda huo usiporudisha kwa hiari nyumba hii basi namuelekeza Kamishna wa Ardhi Mkoa wa Dar es Salaam kushirikiana na vyombo vya usalama ili uondolewe kwa nguvu na Mama huyu apate haki yake,” Amesema Mhe. Ndejembi.
Waziri Mhe. Ndejembi amesisitiza kuwa Serikali ya awamu ya sita itaendelea kulinda maslahi na haki za wananchi wake na haitokubali kuona mtu yeyote anaonewa wala kukosa haki yake kwa sababu ya maslahi binafsi ya mtu yeyote.