Habari

WATUNZA KUMBUKUMBU WATAKIWA KUWA WAAMINIFU NA KUTUNZA SIRI ZA OFISI

  • 24 Sep, 2026
WATUNZA KUMBUKUMBU WATAKIWA KUWA WAAMINIFU NA KUTUNZA SIRI ZA OFISI

Watumishi wa Kada ya Watunza Kumbukumbu na Nyaraka Serikalini wametakiwa kuwa waaminifu, kutunza siri za ofisi na kuendelea kuzingatia maadili ya utumishi wa umma ili kutekeleza majukumu yao kwa weledi.

 

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhandisi Anthony Sanga Septemba 24, 2026 katika Makao Makuu ya Wizara Mtumba, Jijini Dodoma alipokutana na watumishi wa kada hiyo ambao wanafanyakazi katika Ofisi zilizo chini ya Wizara ya Ardhi katika Mikoa mbalimbali nchini waliofika Dodoma kwa ajili ya kushiriki Mkutano Mkuu wa 14 wa Chama cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA).

 

Wakiwa katika kikao hicho ambacho kilichohudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu Bi. Lucy Kabyemera pamoja na Viongozi wa Utawala na Rasilimaliwatu, Mhandisi Sanga amewasisitiza watumishi hao kutambua kuwa wote ni sehemu muhimu ya Wizara, akieleza kuwa kila mtumishi ana mchango katika kuhakikisha Wizara inatekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

 

“Popote ulipo tunakujali, sisi wote ni sawa katika utumishi, bila nyinyi hakuna ofisi hivyo endeleeni kufanya kazi kwa uaminifu na kuhakikisha taarifa na nyaraka za ofisi zinatunzwa kwa kuzingatia taratibu na kanuni za utumishi wa umma.” alisema Mhandisi Sanga.

 

Katibu Mkuu Sanga amesisitiza kuwa katika kipindi ambacho utunzaji wa nyaraka unaendelea kuhamia kwenye mifumo ya kidijitali, watumishi wa kada hiyo wanapaswa kuongeza ujuzi na maarifa ili kuendana na maendeleo ya teknolojia na mahitaji ya sasa ya utendaji kazi.

 

Kwa upande wake Zebedayo Ndahani mtumishi kutoka Baraza la Ardhi na Nyumba Wilaya ya Arumeru Mkoa wa Arusha amewashukuru Viongozi wa Wizara ya Ardhi kwa kuwezesha ushiriki wao katika Mkutano huo na kuahidi kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi.