Habari
WATUMISHI WIZARA YA ARDHI WASISITIZWA KUONGEZA NGUVU UTOAJI ELIMU MATUMIZI YA MFUMO WA e-ARDHI
- 19 Nov, 2026
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Kaspari Kasperi Mmuya, amewataka watumishi wa sekta ya Ardhi katika Ofisi ya Ardhi Mkoa wa Dodoma na Halmashauri zake kuongeza nguvu katika kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi ya Mfumo wa e-Ardhi ili kuwawezesha kutumia mfumo huo katika kupata huduma za ardhi kwa urahisi.
Mhe. Mmuya ametoa wito huo Novemba 18, 2026, jijini Dodoma wakati wa kikao kazi kati yake na watumishi hao, akisisitiza umuhimu wa wananchi kufahamu namna mfumo huo unavyofanya kazi na jinsi unavyorahisisha upatikanaji wa huduma.
"Mfumo wa e-Ardhi ni nyenzo muhimu katika kuboresha utoaji wa huduma za ardhi kwa kutumia teknolojia ya kidijiti, hivyo watumishi wanapaswa kuhakikisha wananchi wanapata uelewa wa kutosha kuhusu matumizi yake". Amesema
Kwa mujibu wa Mhe. Mmuya, elimu hiyo itasaidia wananchi kufahamu namna ya kutumia mfumo wa e-Ardhi katika kuwasilisha na kufuatilia maombi ya huduma za ardhi kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa, badala ya kutegemea kwenda ofisi za ardhi mara kwa mara kwa ajili ya kupata hiduma.
"Matumizi ya Mfumo wa e-Ardhi yana mchango katika kupunguza foleni na msongamano katika ofisi za ardhi, kupunguza muda wa kusubiri huduma na kuondoa usumbufu usio wa lazima kwa wananchi". Ameeleza Mhe. Mmuya
Aidha, amewataka watumishi wa sekta ya ardhi kuwa karibu na wananchi na kutoa maelekezo sahihi kuhusu namna ya kujisajili, kutumia na kufuatilia huduma kupitia Mfumo wa e-Ardhi, pamoja na kuwasaidia wale wanaokutana na changamoto wakati wa kuutumia.
Amesisitiza elimu hiyo ya e-Ardhi itolewe kwa lugha rahisi na kwa njia zinazofikika kwa wananchi wa makundi mbalimbali ili kuhakikisha hakuna mwananchi anayekosa fursa ya kutumia mfumo huo kutokana na kukosa taarifa au uelewa wa namna ya kuutumia.
"Kwa kufanya hivyo, wananchi wataweza kuelewa huduma zinazopatikana kupitia mfumo huo, taratibu za kuzifuata na namna ya kufuatilia hatua za maombi yao". Amesema
Amehitimisha wito wake kwa kuwataka watumishi wa sekta ya ardhi kuhakikisha mfumo huo unafahamika na kutumiwa ipasavyo ili kutimiza lengo la kurahisisha upatikanaji wa huduma, kuongeza ufanisi katika utendaji na kupunguza usumbufu kwa wananchi wanaohitaji huduma za ardhi nchini.