Habari

WATUMISHI WIZARA YA ARDHI WASHIRIKI BONANZA LA SHIMIWI, WATUMISHI WA UMMA WAHAMASISHWA KUSHIRIKI MICHEZO KWA AFYA

  • 18 Aug, 2026
WATUMISHI WIZARA YA ARDHI WASHIRIKI BONANZA LA SHIMIWI, WATUMISHI WA UMMA WAHAMASISHWA KUSHIRIKI MICHEZO KWA AFYA

Watumishi wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi leo tarehe 25 Agosti 2026 wameshiriki Bonanza la Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara, Idara za Serikali na Mikoa (SHIMIWI), lililofanyika katika Uwanja wa John Merlini jijini Dodoma, huku watumishi wa umma wakihamasishwa kuendelea kushiriki michezo kwa ajili ya kuimarisha afya na umoja

 

Akifungua bonanza hilo , Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Juma Mkomi, amesema michezo ni sehemu muhimu ya kujenga afya bora ya mwili na akili, kuimarisha mshikamano na mahusiano baina ya watumishi, pamoja na kuongeza ari na ufanisi katika utendaji wa kazi.

 

Amesema, ushiriki wa watumishi katika michezo mbalimbali unapaswa kuwa sehemu ya utamaduni wa Utumishi wa Umma, kwa kuwa michezo husaidia kupunguza msongo wa mawazo, kujenga udugu na kuongeza nguvu na ari ya kutekeleza majukumu kwa ufanisi.

 

“Ni vyema watumishi wakaendelea kujenga utamaduni wa kushiriki michezo mbalimbali ili kujiongezea afya na kuimarisha mshikamano na mahusiano mazuri baina ya watumishi wa umma,” amesema Mkomi.

 

Katika bonanza hilo, watumishi wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi walishiriki kikamilifu katika michezo mbalimbali, wakionesha nidhamu na mshikamano katika kuiwakilisha Wizara.

 

Aidha, Mkomi amewataka watumishi wanaoshiriki mashindano hayo kuzingatia weledi, maadili, nidhamu na kanuni za Utumishi wa Umma, akisisitiza kuwa ushindani wa michezo unapaswa kwenda sambamba na kuheshimiana na kuzingatia misingi ya uadilifu.

 

Amesema, mashindano hayo pia yanaendelea kujenga mshikamano miongoni mwa watumishi wa umma na kuwaandaa kushiriki mashindano ya kitaifa yatakayofanyika mkoani Kilimanjaro kuanzia Septemba 20 hadi Oktoba 7, 2026.

 

Mashindano hayo yanafanyika chini ya kaulimbiu “SHIMIWI Tupo Tayari Kushiriki AFCON 2027,” ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha watumishi kushiriki kikamilifu katika michezo na kujenga taifa lenye watumishi wenye afya, nguvu na ari ya kulitumikia Taifa.