Habari

WATUMISHI WAHIMIZWA KUJENGA UTAMADUNI WA KUFANYA MAZOEZI

  • 31 Aug, 2026
WATUMISHI WAHIMIZWA KUJENGA UTAMADUNI WA KUFANYA MAZOEZI

Watumishi nchini wamehimizwa kuendeleza utamaduni wa kufanya mazoezi kwa lengo la kujenga na kudumisha afya pamoja na utimamu wa mwili na akili, jambo litakalowawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.

 

Kauli hiyo imetolewa leo, Agosti 29, 2026, na Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Daniel Sillo (MB), wakati akifunga bonanza hilo lililofanyika katika Viwanja vya John Merlin, Halmashauri ya Jiji la Dodoma, ambapo watumishi kutoka Wizara ya Ardhi walishiriki katika bonanza hilo.

 

Mhe. Sillo amesema kuwa mazoezi ni mojawapo ya njia muhimu za kuuweka mwili katika hali nzuri ya utimamu wa afya, hivyo kila mtumishi anapaswa kuwa na utamaduni wa kufanya mazoezi ambapo utimamu wa mwili na akili humwezesha mtumishi kutoa huduma bora kwa wananchi kama ilivyokusudiwa.

 

"Utimamu wa mwili na akili humwezesha mtumishi kutoa huduma bora kwa wananchi,” amesema Mhe. Sillo.

 

Aidha, ameeleza kuwa NMB–Bunge Bonanza 2026 ni sehemu ya shughuli zinazotoa ujumbe kwa Watanzania na jumuiya ya kimataifa kwamba Tanzania iko tayari kushiriki na kuwa mwenyeji wa matukio makubwa ya michezo, pia linaimarisha ushirikiano, mshikamano, afya na mahusiano mema miongoni mwa taasisi na watumishi kupitia michezo.

 

Katika bonanza hilo, timu ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ardhi FC, imeendelea kuonyesha uwezo wake baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3–0 dhidi ya timu ya Bunge FC.

 

Sambamba na hayo, Mhe. Sillo amesema Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuboresha miundombinu ya michezo nchini, hatua inayolenga pia kujiandaa na mashindano ya AFCON 2026.

 

Ushiriki wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi katika bonanza hilo unaendelea kusisitiza umuhimu wa michezo katika kujenga afya bora, kuimarisha mshikamano na kuongeza ufanisi wa watumishi katika utekelezaji wa majukumu yao.