Habari
WATU WOTE WANA HAKI YA KUMILIKI ARDHI : NAIBU WAZIRI KASPAR MMUYA
- 04 Mar, 2026
Katika Kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake duniani NAIBU WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Kaspar Mmuya amesema kila mtu anayohaki ya kumiliki ardhi kwa mujibu wa sheria za nchi.
Naibu Waziri Mmuya amesema hayo mkoani Manyara leo tarehe 03 Machi 2026 alipotembelea Kliniki ya Ardhi ijulikanayo kama Samia Ardhi Kliniki inayoendelea katika ofisi za kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Manyara.
"Mwanamke asionekane anamiliki ardhi kwa kuzingatia mila na desturi za kabila lake hapana, sheria ndio iongoze katika kumpa haki yake" amesema Naibu waziri Kaspar Mmuya.
Ameongeza kuwa maboresho ya Sera ya Ardhi ya Mwaka 2023 yamelenga kutoa usawa kwa kila mtu kumiliki ardhi mathalani wanawake ambao mifumo ya kiimla imekuwa ikiwaminya wanawake katika haki ya kumiliki ardhi zao.
Kwa upande wake Mpima ardhi wa halmashauri ya Mji wa Babati Bi. Ploskovia Lambert Luta amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika kliniki hiyo ili waweze kupatiwa hatimiliki zao wakiwa na Nyaraka Stahiki .
Naye Bi. Fatuma Abdallah Bakari Mkazi wa Hangoni C Wilayani Babati Mkoani Manyara ameishukuru Serikali kwa kuwapa kipaumbele wanawake katika kumiliki ardhi ikiwa ni utekelezaji wa Sera ya Ardhi toleo la 2023.
Zoezi la Samia Ardhi Kliniki linaendelea katika mikoa yote nchini kuelekea maadhimisho ya siku ya wanawake duniani likilenga kutoa hamasa kwa wanawake nchini kuweza kumiliki ardhi kwa kupatiwa hatimiliki.