Habari

WATENDAJI ARDHI WATAKIWA KUTOCHELEWESHA HUDUMA KWA MAKUSUDI

  • 02 Feb, 2025
WATENDAJI ARDHI WATAKIWA KUTOCHELEWESHA HUDUMA KWA MAKUSUDI

Serikali imewataka watendaji wa sekta ya Ardhi nchini kutochelewesha huduma za sekta ya Ardhi kwa makusudi wakati wanapowahudumia wananchi wanaokwenda kupata huduma katika ofisi zao.

Hayo yameelezwa Januari 31, 2025 mkoani Iringa na Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bw. Hamdouny Mansoor wakati wa kikao kazi cha watumishi wa sekta ya Ardhi Mkoa wa Iringa.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Mhandisi Anthony Sanga, Bw. Mansoor amesema kumekuwa na ucheleweshaji huduma kwa makusudi na wakati mwingine watendaji wa sekta ya Ardhi kuwatuma mwananchi wanaokwenda kupata huduma.

Aidha, Mansoor kupitia kikao hicho kilichoandaliwa na Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Iringa ametaka kuwekwa utaratibu rasmi katika ofisi zote za Ardhi kuanzia ngazi ya wilaya wa namna ya kupata hati ili wananchi wauelewe na kuufuata utaratibu huo.

Katibu Tawala Msasizi Mkoa wa Iringa amesema kupitia kikao hicho kuwa, kutokana na migogoro inayoendelea ya ardhi na kuratibiwa na ofisi ya mkoa na wilaya ziwepo kumbukumbu za utatuzi wa ile migogoro iliyomalizika ili kuwasaidia viongozi wanaoitisha majalada kwa lengo la kujua hatua zilizochukuliwa.

Kwa upande wake Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Iringa Bw. Frank Minzikuntwe ameeleza kuwa, kikao kilichofanyika cha watumishi kilikuwa na lengo la kuzungumza na kupeana mikakati pamoja na mipango kazi ya namna ya kushughulikia kero na utoaji huduma za sekta ya ardhi kwa haraka zaidi.

Kikao hicho cha siku moja kimeshirikisha watendaji wa sekta ya ardhi kutoka halmashauri zote za mkoa wa Iringa pamoja na wale wa Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Iringa.