Habari

WATAALAMU WABAINI UENDELEZAJI ARDHI BAADA YA KATAZO LA KUENDELEZA MAENEO KATIKA ZOEZI LA UTHAMINI WA SGR KIGOMA

  • 26 Aug, 2026
WATAALAMU WABAINI UENDELEZAJI ARDHI BAADA YA KATAZO LA KUENDELEZA MAENEO KATIKA ZOEZI LA UTHAMINI WA SGR KIGOMA

Wataalamu kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia Ofisi ya Mthamini Mkuu wa Serikali wamebaini ukwiukwaji wa taratibu kwa baadhi ya wananchi kwa kuendelea kufanya uendelezaji wa ardhi na mali zao baada ya kutolewa kwa katazo la kuendeleza maeneo hayo.

 

Akieleza changamoto hiyo Agosti 22, 2026 katika Kijiji cha Mwamila kilichopo katika kata ya Kazuramimba Mkoani Kigoma, Mthamini Kiongozi wa mradi, Rashid Magetta amesema baadhi ya wananchi wameendelea kufanya maboresho ya mali zao baada ya katazo, ikiwemo kuendelea na ujenzi, kwa lengo la kuongeza thamani ya mali hizo katika mchakato wa fidia.

 

“Wananchi wanapaswa kuzingatia katazo lililotolewa na kutofanya maendeleo mapya katika maeneo yanayohusika na uthamini,” amesema Magetta.

 

Timu ya Kitengo cha Habari cha Wizara iliyofika Kijiji cha Mwamila na kushuhudia baadhi ya maeneo ambayo yalikuwa yakiendelea kufanyiwa maboresho baada ya katazo la Agosti 18, 2026, ikiwemo ujenzi wa msingi wa nyumba ambao bado haujakamilika pamoja na maboresho katika baadhi ya nyumba zilizopo.

 

Miongoni mwa wananchi waliokiri kufanya maboresho baada ya katazo ni Bi. Agnes Maduhu, ambaye alisema aliendelea na ujenzi licha ya katazo na kutoa wito kwa wananchi wengine kuzingatia maelekezo yaliyotolewa na wataalamu.

 

Naye Bi. Asia Saidi alikiri kufanya maboresho katika nyumba yake, ikiwemo kupaka rangi na kuweka vioo vya madirisha, akieleza kuwa alifanya hivyo kwa lengo la kuongeza thamani ya mali yake katika mchakato wa fidia.

 

Kwa mujibu wa bwana Magetta, uendelezaji wa Ardhi au mali baada ya kutolewa kwa katazo hauwezi kuchukuliwa kama msingi wa kuongeza thamani ya fidia, badala yake unakiuka taratibu zinazotumika katika mchakato wa uthamini.

 

Amesisitiza kuwa wananchi wanapaswa kusubiri kukamilika kwa hatua za uthamini na kufuata maelekezo yanayotolewa na wataalamu ili kuepusha changamoto katika mchakato wa fidia.

 

Wizara imeendelea kuwataka wananchi kushirikiana na wataalamu wakati wa zoezi hilo, kutoa taarifa sahihi kuhusu maeneo na mali zao na, muhimu zaidi, kuzingatia katazo la kufanya maendeleo mapya baada ya zoezi la uthamini kuanza.