Habari
WATAALAMU WA MIPANGOMIJI NA WATHAMINI WASISITIZWA KUSIMAMIA MAADILI YA TAALUMA
- 21 Oct, 2026
Kamati ya Ardhi Maliasili na Utalii imepokea na kujadili taarifa za Bodi ya Usajili wa Wataalamu wa Mipangomiji (TPRB) na Bodi ya Usajili wa Wathamini (VRB) ambazo zipo chini Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na kusisitiza Wizara hiyo iendelee kushirikiana na bodi hizo na kuzijengea uwezo ili ziendelee kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia maadili ya taaluma zao.
Akizungumza kwa niaba ya Kamati hiyo Mwenyekiti Mhe. Timotheo Mzava amesema bodi hizo zinajukumu la kuangalia na kuzifanyia kazi changamoto zinazowakumba wananchi ili kuleta tija iliyokusudiwa.
Aidha, Mhe. Mzava amezitaka bodi hizo ziendelee kuboresha usimamizi wa wataalamu kupitia mifumo ya kidijiti ili kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia.
Kwa upande wake Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo amesema wizara yake imepokea maelekezo ya kamati na watayafanyia kazi.
Amesisitiza wizara yake itaendelea kusimamia bodi hizo ili kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia weledi na maadili ya taaluma zao ili kutoa huduma bora kwa wananchi kwa wakati.
Dkt. Akwilapo aliambatana na Naibu Waziri wake Mhe. Kaspar Mmuya, Katibu Mkuu Mhandisi Anthony Sanga, Wajumbe wa Menejimenti ya Wizara pamoja na wataalamu kutoka bodi hizo.