Habari
WASAJILI WA HATI WASAIDIZI WATAKIWA KUZINGATIA MAADILI NA KUIMARISHA HUDUMA KWA WANANCHI
- 12 Oct, 2026
Wasajili wa Hati Wasaidizi kutoka mikoa mbalimbali nchini wametakiwa kuzingatia maadili ya Utumishi wa Umma, kuimarisha weledi na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi ili kuhakikisha usimamizi na usajili wa hati za ardhi unafanyika kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.
Wito huo umetolewa na Msajili wa Hati kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bw. David Mushendwa, wakati akifungua mkutano wa Wasajili wa Hati Wasaidizi Oktoba 9, 2026 jijini Arusha.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Bw. Mushendwa amewahimiza washiriki kuwa wasikivu, kushiriki kikamilifu katika majadiliano na kutumia fursa hiyo kujifunza masuala mbalimbali yatakayowawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.
Amesema mkutano huo ni sehemu ya utaratibu wa Kitengo cha Msajili wa Hati wa Wizara wa kukutana na Wasajili wa Hati Wasaidizi kutoka mikoa mbalimbali nchini kila mwaka wa fedha wa Serikali, kwa lengo la kutathmini utekelezaji wa majukumu ya mwaka uliopita, kubaini changamoto na kuweka mikakati ya kuboresha utendaji katika mwaka wa fedha unaofuata.
Kwa mujibu wa Bw. Mushendwa, mkutano huo unatoa fursa ya kubadilishana uzoefu na maarifa miongoni mwa wataalamu hao, hatua inayolenga kuimarisha utendaji wa kitengo na kuboresha huduma za usajili wa hati zinazotolewa kwa wananchi.
Katika siku ya kwanza ya mkutano huo, washiriki wamepatiwa mada kuhusu Maadili ya Utumishi wa Umma pamoja na taratibu za usajili wa hati za sehemu ya jengo, kwa lengo la kuongeza uelewa na kuhakikisha utekelezaji sahihi wa majukumu hayo kwa kuzingatia miongozo husika.
Kwa upande wake, mtoa mada kuhusu Maadili ya Utumishi wa Umma Afisa Rasiliamaliwatu Mwandamizi kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Hassan Kilenza, amewataka Wasajili hao kuzingatia misingi ya maadili katika utekelezaji wa majukumu yao, ikiwemo kutunza siri na kulinda usiri wa taarifa za Serikali.
Bw. Kilenza amesisitiza umuhimu wa watumishi kufanya kazi kwa uadilifu, kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya utumishi wa umma ili kulinda heshima na hadhi ya utumishi wa umma pamoja na kuimarisha imani ya wananchi kwa Serikali.
Aidha, amewakumbusha watumishi wa umma kuzingatia mipaka ya mamlaka waliyopewa, kutumia kwa uangalifu vifaa na rasilimali za Serikali, kusimamia matumizi sahihi ya fedha za umma na kuepuka vitendo vinavyoweza kusababisha upotevu au uharibifu wa mali za Serikali, ikiwemo matumizi yasiyo sahihi ya magari ya Serikali.
Mkutano huo unafanyika kwa siku mbili kuanzia Otoba 9 hadi 10, 2026 unaendelea jijini Arusha, ukiwa na lengo la kuimarisha weledi, uwajibikaji na ufanisi wa Wasajili wa Hati Wasaidizi katika kutekeleza majukumu yao ya kusajili hati na kutoa huduma bora kwa wananchi.