Habari
WASAJILI WA HATI WASAIDIZI WATAKIWA KUTUMIA MIFUMO YA e-ARDHI NA e-OFFICE KWA UFANISI ILI UBORESHA UTOAJI WA HUDUMA KWA WANANCHI
- 12 Oct, 2026
Wasajili wa Hati Wasaidizi kutoka mikoa mbalimbali nchini wametakiwa kutumia mifumo ya kielektroniki ikiwemo e-Ardhi na e-Office katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuongeza ufanisi, kuondoa urasimu na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bi. Salome Cyril Kessy, mkoani Arusha wakati akizungumza na wasajili hao katika siku ya mwisho ya kikao kazi chao, ambapo amesisitiza umuhimu wa kuzingatia kanuni, taratibu, miongozo na maadili ya Utumishi wa Umma katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.
Amesema matumizi ya mifumo ya kielektroniki yanapaswa kwenda sambamba na uzingatiaji wa misingi ya uongozi bora, nidhamu kazini, mavazi yanayozingatia taratibu za kiutumishi na uwajibikaji katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na kwa wakati.
Aidha, amewataka watumishi hao kuzingatia maadili ya utumishi wa umma ili kujenga imani ya wananchi kwa taasisi za Serikali na kuhakikisha huduma zinazotolewa zinaendana na viwango vinavyotakiwa.
Kwa upande wake, Msajili wa Hati kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bw. David Mushendwa, amewataka Wasajili wa Hati Wasaidizi kuongeza juhudi katika utekelezaji wa majukumu yao ili kufikia malengo yaliyowekwa na Wizara, huku wakihakikisha mifumo ya utoaji huduma inakuwa rafiki kwa wananchi na kupunguza changamoto zinazoweza kusababisha ucheleweshaji wa huduma.
Amesema ni vyema katika kutekeleza majukumu yao kufanya kwa ufanisi na weledi na kuondoa urasimu, kuimarisha usimamizi wa watumishi na kutoa motisha kwa wafanyakazi wanaofanya vizuri, pamoja na kuwaandaa viongozi wa baadaye watakaosaidia kuimarisha utendaji kazi ndani ya taasisi.
Bw.Mushendwa amesema viongozi wanapaswa kujenga tabia bora za kiuongozi, zikiwemo kuwasikiliza watumishi, kufafanua masuala mbalimbali kwa kina, kushughulikia changamoto kwa wakati, kugawa majukumu kwa ufanisi na kuheshimu kila mtumishi katika eneo la kazi.
Aidha, amewataka viongozi hao kulinda ustawi wa watumishi na kujenga mazingira bora ya kazi yatakayochochea uwajibikaji, ushirikiano na ufanisi katika utoaji wa huduma za ardhi kwa wananchi.
Kikao kazi hicho kilichofanyika kuanzia tarehe 9 hadi 10 Oktoba 2026 ni sehemu ya juhudi za Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi za kuimarisha utendaji wa Wasajili wa Hati Wasaidizi, kuongeza matumizi ya mifumo ya kidijitali na kuboresha huduma za usajili wa hati nchini.