Habari

WASAJILI WA HATI WASAIDIZI WAMETAKIWA KUTOA HUDUMA BORA KWA WANANCHI,KUEPUKA URASIMU NA KUTUMIA MIFUMO YA TEHAMA KATIKA KUTOA HUDUMA KWA HARAKA

  • 12 Oct, 2026
WASAJILI WA HATI WASAIDIZI WAMETAKIWA KUTOA HUDUMA BORA KWA WANANCHI,KUEPUKA URASIMU NA KUTUMIA MIFUMO YA TEHAMA KATIKA KUTOA HUDUMA KWA HARAKA

Wasajili wa Hati Wasaidizi kutoka mikoa mbalimbali nchini wametakiwa kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wananchi kwa kuzingatia weledi, uadilifu na uwajibikaji, huku wakiepuka vitendo vya urasimu na upendeleo katika utekelezaji wa majukumu yao.

 

Wito huo umetolewa Oktoba 10, 2026, na Msajili wa Hati wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bw. David Mushendwa, wakati akizungumza na Wasajili wa Hati Wasaidizi katika kikao kazi kilichofanyika katika Ukumbi wa Point Zone Resort, mkoani Arusha.

 

Akizungumza katika kikao hicho, Bw. Mushendwa amewataka Wasajili hao kuhakikisha wanatatua changamoto zinazowakabili wananchi kwa wakati, kuimarisha mahusiano mazuri kati ya watumishi na wananchi, pamoja na kuondoa mianya ya upendeleo katika utoaji wa huduma za usajili wa hati.

 

Aidha, amewahimiza kutumia redio za kijamii katika maeneo yao kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala ya usajili wa hati na huduma mbalimbali zinazotolewa na Wizara, ili kuongeza uelewa wa wananchi na kuwawezesha kupata huduma kwa urahisi.

 

Amesisitiza kuwa Wasajili wa Hati Wasaidizi wana wajibu wa kuhakikisha huduma zinazotolewa katika ofisi zao zinaendana na malengo ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ya kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi, kuongeza uwazi na kuimarisha uwajibikaji.

 

Pia, amewataka kujenga mazingira bora ya utendaji kazi, kushughulikia migogoro inayojitokeza baina ya wananchi na watumishi kwa kuzingatia sheria, taratibu na misingi ya haki, pamoja na kuhakikisha kila mwananchi anahudumiwa bila ubaguzi wala upendeleo.

 

Kikao kazi hicho kimewakutanisha Wasajili wa Hati Wasaidizi kutoka mikoa mbalimbali nchini kwa lengo la kujadili masuala ya kiutendaji na kuimarisha ufanisi katika utoaji wa huduma za usajili wa hati kwa wananchi.