Habari
WASAJILI WA HATI NCHINI WAJIPANGA KWA MATUMIZI YA TEHAMA
- 21 Jul, 2025

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia Kitengo cha Hati, imeendesha kikao kazi cha siku mbili kilichowakutanisha Wasajili wa Hati Wasaidizi kutoka mikoa mbalimbali nchini, kwa lengo la kujadili na kujipanga kwa matumizi ya TEHAMA katika shughuli za usajili.
Aidha, kikao hicho pia kimepitia utekelezaji wa Mpango Kazi wa mwaka 2024/25 na kuweka mikakati ya kufanikisha malengo ya mwaka 2025/26.
Akizungumza katika kikao hicho, Msajili wa Hati nchini, Ndg. David Mushendwa alisisitiza umuhimu wa kutumia TEHAMA ili kuongeza ufanisi, uwazi, na kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Alieleza kuwa, utekelezaji wa Mpango Kazi wa mwaka ujao unapaswa kuendana na mageuzi ya kidijitali yanayolenga kuboresha utendaji kazi wa Sekta ya Ardhi.
Msajili huyo pia aliwakumbusha Wasajili wa Hati Wasaidizi kuhusu wajibu wao kama maafisa wa serikali kuzingatia maadili ya utumishi wa umma.
"Msiruhu mianya ya rushwa, fanyeni kazi kwa haki, usawa na kwa kuzingatia maslahi ya wananchi". Alisema
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa Wizara ya Ardhi Bi. Prisca B. Lwangili, aliwahimiza washiriki wa kikao kufanya kazi kwa weledi, bidii na uadilifu.
Kwa mujibu wa Bi. Prisca, utoaji wa huduma bora za usajili wa miamala mbalimbali unategemea kiwango cha uwajibikaji wa watumishi na matumizi sahihi ya mifumo ya TEHAMA.
Naye Emmanuel Gwaltu, Msajili wa Hati Msaidizi Mkoa wa Shinyanga ambaye ni miongoni mwa washiriki wa kikao hicho, alisema kuwa mafunzo hayo ya kidijitali yatawasaidia kuboresha utendaji kazi wao kwa kupunguza msongamano wa hati katika ofisi, kurahisisha upatikanaji wa hati kwa wananchi, na kuhifadhi kumbukumbu kwa njia ya kisasa na salama.
Kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa Point Zone Resort, mkoani Arusha kuanzia tarehe 18 hadi 19 Julai, 2025..