Habari

WAPIMA ARDHI WATAKIWA KUBUNI MFUMO WA KUBAINISHA VIWANJA VISIVYOKUWA NA HATI MILIKI

  • 20 Nov, 2026
WAPIMA ARDHI WATAKIWA KUBUNI MFUMO WA KUBAINISHA VIWANJA VISIVYOKUWA NA HATI MILIKI

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Kaspar Mmuya, amewataka Wapima Ardhi nchini kushirikiana na Wizara kubuni mfumo utakaosaidia kubainisha viwanja ambavyo havina hati miliki ili kurahisisha usimamizi wa milki za ardhi na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

 

Mhe. Mmuya ametoa wito huo leo tarehe 19 Novemba 2026, jijini Mwanza, wakati akifungua Kongamano la Wapima Ardhi Tanzania pamoja na Mkutano Mkuu wa 30 wa Mwaka wa Taasisi ya Wapima Ardhi Tanzania (IST).

 

Amesema Wizara haitavumilia ucheleweshaji wa aina yoyote katika uandaaji na utoaji wa hati miliki za ardhi unaosababishwa na uzembe wa watumishi wa sekta hiyo, akisisitiza kuwa wananchi wanapaswa kupata huduma kwa wakati na kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa.

 

Aidha, amewasihi Wapima Ardhi kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika kubuni na kutekeleza maboresho ya mfumo wa upimaji nchini ili kuwezesha ardhi ya nchi kupimwa na wananchi kupata huduma bora zinazohusiana na umiliki wa ardhi.

 

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Mhe. Amir Mkalipa, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza CP Salum Rashid Hamduni, amesema mkoa huo unaendelea kutekeleza upimaji shirikishi wa ardhi pamoja na kutenga maeneo kwa ajili ya kongani za viwanda katika maeneo ya Wilaya za Misungwi na Magu, hatua inayolenga kuwezesha matumizi bora ya ardhi na kuimarisha shughuli za maendeleo.

 

Naye Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bw. Hamdouny Mansoor, amesema Wizara inatarajia kuanzisha mfumo wa upimaji wa kielektroniki unaoitwa Coneta, utakaowawezesha wapima ardhi kutumia teknolojia katika kupata majira na nukta za maeneo wanayoyapima, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha miundombinu na huduma za upimaji nchini.

 

Kongamano la mwaka huu limeongozwa na kauli mbiu isemayo "Sayansi ya Kijiografia, Akili Unde na Upimaji Ardhi wa Kisasa: Kuchochea Ubunifu kwa ajili ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050".