Habari

WANAWAKE SINGIDA WAHAMASISHWA KUMILIKI HATI: OMBI LA TOLEWA KUANZISHA SOMO LA ARDHI NA KLABU ZA ARDHI MASHULENI

  • 04 Mar, 2026
WANAWAKE SINGIDA WAHAMASISHWA KUMILIKI HATI: OMBI LA TOLEWA KUANZISHA SOMO LA ARDHI NA KLABU ZA ARDHI MASHULENI

Wanawake mkoani Singida wamehimizwa kujitokeza kwa wingi kumiliki hati za ardhi ili kulinda na kuhakikisha usalama wa mali zao, katika kongamano maalum la wanawake lililofanyika mkoani humo.

 

Akitoa elimu katika kongamano hilo, Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Singida Bi.Shamim Giza amesema umiliki wa hati ni nguzo muhimu ya kumwezesha mwanamke kiuchumi na kijamii, akieleza kuwa hati inaleta uhakika wa kisheria na kuondoa migogoro isiyo ya lazima.

 

Amesisitiza kuwa mwanamke mwenye hati anakuwa na nguvu ya maamuzi juu ya rasilimali yake, anaweza kuitumia kama dhamana kupata mikopo na kuwekeza kwa maendeleo ya familia na jamii kwa ujumla.

 

Aidha Bi.Shamim kupitia kongamano hilo ameiomba Serikali, kupitia Mbunge wa Singida Mjini, kupeleka marekebisho ya Sheria Bungeni ili kuruhusu kuanzishwa kwa somo la Ardhi mashuleni ili watoto waanze kupata maarifa ya masuala ya ardhi mapema.

 

Amependekeza kuanzishwa kwa klabu za Ardhi mashuleni zitakazowajengea wanafunzi uelewa na kuwalea kuwa mabalozi wa ardhi na wamiliki halali wa baadaye.

 

Elimu hiyo imetolewa ikiwa ni mwendelezo wa programu ya Samia Ardhi Kliniki inayoendelea mkoani Singida, yenye lengo la kusogeza huduma za ardhi karibu na wananchi na kuongeza uelewa kuhusu haki na wajibu katika umiliki wa ardhi.

 

Kongamano hilo limekuwa chachu ya mabadiliko kwa wanawake wengi waliohudhuria, huku wakiapa kuwa mabalozi wa kuhamasisha wenzao kujitokeza kupata hati na kushiriki kikamilifu katika masuala ya ardhi kwa maendeleo endelevu ya taifa.