Habari
WANAWAKE MTWARA WAIPOKEA KWA SHAUKU KLINIKI YA ARDHI KIDIJITI
- 24 Sep, 2026
Wanawake mkoani Mtwara wameendelea kujitokeza kwa wingi katika Kliniki ya Ardhi Kidijiti inayofanyika katika Uwanja wa Mashujaa Park, wakifuatilia huduma mbalimbali za ardhi ikiwemo maendeleo ya hati zao.
Kliniki hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi za kusogeza huduma za ardhi karibu na wananchi, pamoja na kuwawezesha kupata huduma kwa urahisi na kwa wakati kupitia mifumo ya kidijiti.
Akizungumza baada ya kupata huduma katika Kliniki hiyo, Bi. Sofia Yusufu Mwingira amepongeza hatua hiyo, akisema huduma zinazotolewa zimekuwa na manufaa kwa wananchi na kuishukuru Serikali kwa kuwasogezea huduma karibu.
Kwa upande wake, Bi. Maria Agustino amewahimiza wananchi, hususan wanawake, kujitokeza kwa wingi kutumia fursa hiyo na kufuatilia huduma zao za ardhi.
Wananchi wametakiwa kuendelea kujitokeza katika Kliniki ya Ardhi Kidijiti iliyoanza nchi nzima ili kupata huduma na taarifa mbalimbali za ardhi, kuelekea uzinduzi wa Ardhi Kidijiti unaotarajiwa kufanyika mkoani Mtwara tarehe 25 Septemba 2026 .
Mgeni rasmi katika uzinduzi huo anatarajiwa kuwa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya makazi Dkt. Leonard Akwilapo.