Habari

WANAWAKE DODOMA WAPATA TABASAMU KUPITIA SAMIA ARDHI KLINIKI

  • 07 Mar, 2026
WANAWAKE DODOMA WAPATA TABASAMU KUPITIA SAMIA ARDHI KLINIKI

Wanawake katika Mkoa wa Dodoma wameendelea kupata tabasamu baada ya kunufaika na huduma mbalimbali za masuala ya ardhi zilizotolewa kupitia Samia Ardhi Kliniki ikiwa ni mpango maalumu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi unaolenga kuwafikia wanawake ili kuwape elimu ya masuala mbalimbali ya ardhi.

 

Akizungumza katika kliniki hiyo tarehe 7 Machi 2026, Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Dodoma Bi. Happiness Mtutwa amesema kuwa, Samia Ardhi Kliniki imekuwa fursa muhimu kwa wanawake kupata elimu na huduma zinazowawezesha kumiliki na kutumia ardhi kwa tija.

 

Amesema, kupitia Kliniki hiyo jumla ya Wanawake 1,916 mkoa wa Dodoma wamepata huduma, hati 694 zimesajiliwa, hati 316 zimekabidhiwa kwa wanawake, migogoro 49 imetatuliwa na wanawake 105 wamepata ushauri bure wa kisheria.

 

"Tunawashukuru sana Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Chama cha Wanawake Wanasheria Tanzania (TAWLA), Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, pamoja Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kwa kushirikiana nasi katika kufanikisha utekelezaji wa programu hii ambapo walitoa huduma bure kwa wananchi waliofika kupata huduma" amesema Mtutwa 

 

Edna Emmanuel Mkazi wa Dodoma amewahimiza wanawake wafike kwa wingi pindi Kliniki hizi zinapotangwaza ili wafuatilie hati kwa kufanya hivyo kutasaidia kuongeza thamani katika maeneo yao.

 

"Ukinunua ardhi usikae na maratasi ndani toka nenda kafuatilie hati yako ili kuongeza usalama wa milki yako" amesema Edna

 

Naye Bi. Leticia Mlolwa Mkazi wa Dodoma ameomba kuongezewa muda kwa Kliniki hii ili kina mama wengi zaidi waweze kujitokeza zaidi. 

 

Samia Ardhi Kliniki ilianza tarehe 2 Machi 2026 na inahitimishwa leo 7 Machi 2026, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.