Habari

WANAWAKE 1,566 WAFIKIWA NA SAMIA ARDHI KLINIKI DODOMA

  • 06 Mar, 2026
WANAWAKE 1,566 WAFIKIWA NA SAMIA ARDHI KLINIKI DODOMA

Jumla ya wanawake 1,566 wamenufaika na huduma mbalimbali za masuala ya ardhi zinazotolewa kupitia Kliniki Maalum ya Wanawake inayojulikana kama Samia Ardhi Kliniki katika Mkoa wa Dodoma.

 

Akizungumza tarehe 06 Machi, 2026 katika Ofisi za Ardhi Mkoa wa Dodoma, Kamishna wa Ardhi Msaidizi wa Mkoa huo, Bi. Happiness Mtutwa, amesema idadi hiyo inaendelea kuongezeka kadri wanawake wanavyojitokeza kupata huduma na elimu kuhusu masuala ya ardhi.

 

“Mpaka sasa wanawake 1,566 wamehudumiwa kupitia Samia Ardhi Kliniki na bado idadi inaendelea kuongezeka kutokana na uhitaji mkubwa wa wanawake kupata usalama wa milki zao pamoja na elimu ya masuala ya ardhi,” amesema Mtutwa.

 

Ameongeza kuwa, kupitia kliniki hiyo wanawake wanapatiwa huduma mbalimbali ikiwemo ushauri wa kitaalamu kuhusu umiliki wa ardhi, utatuzi wa changamoto za ardhi pamoja na elimu ya namna ya kutumia ardhi kama nyenzo ya kuongeza kipato.

 

“Kupitia Samia Ardhi Kliniki, wataalamu wa masuala ya sheria kutoka taasisi na vyama mbalimbali wameshiriki katika kutoa elimu, zikiwemo Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu pamoja na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS),” amesema Mtutwa.

 

Kupitia Ofisi za Makamishna wa Ardhi Wasaidizi wa Mikoa Wizara ya Ardhi imeendelea kusogeza huduma za ardhi karibu na wananchi ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita katika kuhakikisha wanawake wanapata haki ya kumiliki na kunufaika na rasilimali ardhi.

 

Samia Ardhi Kliniki iliyoanza tarehe 2 Machi 2026 inaendelea katika mikoa yote Tanzania Bara na inatarajiwa kuhitimishwa tarehe 7 Machi 2026 ikiwa ni kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, ikiwa na kauli mbiu “Mwanamke; Haki Yako, Miliki Ardhi Sasa.”