Habari

WANAOTEKELEZA KAZI YA UPANGAJI NA UPIMAJI ARDHI MAHOMANYIKA WAPONGEZWA

  • 15 Apr, 2026
WANAOTEKELEZA KAZI YA UPANGAJI NA UPIMAJI ARDHI MAHOMANYIKA WAPONGEZWA

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo, ameipongeza timu ya wataalamu wanaotekeleza kazi ya upangaji na upimaji wa ardhi pamoja na uchambuzi wa nyaraka, kwa kuonesha weledi, ufanisi na kufanya kazi kwa wakati katika mchakato wa kuwapatia wananchi viwanja mbadala.

 

Akizungumza baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa maelekezo yake kuhusu upimaji, upangaji na uhakiki wa taarifa za wananchi wanaostahili kupewa viwanja katika maeneo ya Mahomanyika na Ipala jijini Dodoma, Dkt. Akwilapo alisema juhudi za timu hiyo zinaonyesha dira sahihi ya Serikali katika kutatua changamoto za ardhi.

 

Alisisitiza kuwa, kuendelea kwa ushirikiano na nidhamu ya kazi miongoni mwa wataalamu hao kutasaidia kuharakisha utatuzi wa migogoro ya ardhi na kuwapatia wananchi haki zao kwa wakati.

 

Akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya kazi hiyo, Bi. Anna Paul Nade - Afisa Mipango miji wa Jiji la Dodoma alisema eneo la Mahomanyika lenye ukubwa wa hekta 2,336 (sawa na ekari 5,816.14) ni eneo la Serikali lililotengwa kwa matumizi mbalimbali, likiwemo utoaji wa viwanja mbadala kwa wananchi waliokumbwa na changamoto za ardhi.

 

Alieleza kuwa, kazi ya upangaji na Upimaji katika eneo hilo imelenga kupunguza na kumaliza kabisa migogoro ya ardhi katika Jiji la Dodoma, hususan katika kata za Nzuguni na Ipala.

 

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, katika kipindi cha siku 36 za utekelezaji, jumla ya viwanja 6,779 vimepimwa huku viwanja 4,886 vikiwa tayari vimeidhinishwa. Aidha, jumla ya viwanja vilivyopimwa hadi sasa katika eneo lote la mradi imefikia 9,655.

 

Kwa upande wake, Mpima kutoka Ofisi ya Ardhi Mkoa wa Dodoma, Bw. Remidias Rupia, alisema jumla ya viwanja 5,402 vimepimwa, kati ya hivyo 2,433 vimekamilika kwa maandalizi ya data na 1,786 tayari vimeidhinishwa huku viwanja 1,813 vikiendelea kufanyiwa kazi.

 

Katika hatua nyingine, taarifa ya uchambuzi wa madai ya viwanja mbadala iliyowasilishwa na Afisa Ardhi Mkoa wa Dodoma Bw. Letare Shoo amebainisha kuwa kati ya madai 5,683 yaliyowasilishwa na wananchi, madai 2,624 pekee ndiyo yameonekana kuwa halali baada ya kufanyiwa uchambuzi wa kina uliohusisha nyaraka, majalada, maamuzi ya mahakama pamoja na uhakiki wa maeneo husika.

 

Hatua hiyo inaashiria mafanikio makubwa katika juhudi za Serikali za kuhakikisha haki inatendeka kwa wananchi na migogoro ya ardhi inapatiwa ufumbuzi wa kudumu.