Habari
WANANCHI WATAKIWA KUSITISHA SHUGHULI NDANI YA ENEO LA JUMUIYA YA HIFADHI YA WANYAMAPORI MAKAME
- 26 Oct, 2026
Serikali imewataka wananchi waliopewa maeneo ya kilimo na Kijiji cha Ngaboro ndani ya eneo la Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Makame wilayani Kiteto mkoani Manyara kusitisha shughuli zao kwenye maeneo hayo huku Kijiji cha Ngaboro kikielekezwa kutenga eneo mbadala la kilimo lenye ukubwa wa ekari 1,200.
Hayo yamebainishwa Oktoba 24, 2026 wilayani Kiteto mkoa wa Manyara na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo, wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Ndaleta kuhusu mgogoro wa ardhi uliodumu muda mrefu katika eneo hilo.
Mgogoro huo wa ardhi unahusisha wananchi wa vijiji vya Makame, Ndedo, Ngabolo, Mwitikila na Irkiushiorbor vilivyopo Wilaya ya Kiteto Mkoa wa Manyara na vijiji vya Obloroti, Mrijo juu na Mrijo chini vilivyopo Wilaya ya Chemba Mkoa wa Dodoma.
Mhe. Dkt Akwilapo aliyeambatana na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Hamad Hassan Chande wakati akitoa maelekezo hayo ya Serikali amesema, maeneo yaliyotengwa katika mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji vya Makame, Ishboru, Ndejwa na Katikati yanapaswa kuendelea kutumika kwa madhumuni yaliyokusudiwa.
Aidha, vijiji vinavyounda Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Makame vimetakiwa kuhuisha mipango yao ya matumizi ya ardhi ili iendane na mahitaji ya sasa.
Ameeleza kuwa, baada ya kuhuishwa kwa mipango ya matumizi bora ya ardhi, mipaka ya Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Makame inapaswa kufafanuliwa na kuwekewa alama zinazoonekana wazi ili kuzuia uvamizi na migogoro ya ardhi.
"Viongozi wa vijiji wahakikishe ugawaji wa ardhi unafanyika kwa kuzingatia sheria, mipaka ya kiutawala na mipango ya matumizi ya ardhi", amesema.
Kwa mujibu wa Mhe. Dkt Akwilapo, wananchi wanaodai kupewa maeneo na vijiji vya Ndareta na Mwitikila ndani ya maeneo ya vijiji vya Katikati na Ngaboro wanatakiwa kutambua kuwa maeneo hayo yaligawiwa na mamlaka isiyokuwa na uwezo wa kisheria wa kuyagawa.
Amesema, serikali inatambua umuhimu wa ardhi katika maisha na maendeleo ya wananchi kwa kutatua migogoro ya ardhi inayokwamisha maendeleo katika maeneo mbalimbali nchini jambo alilolieleza linapelekea kuwepo ustawi wa wananchi pamoja na matumizi bora ya ardhi kwa maslahi mapana ya taifa.
Mhe. Akwilapo ameongeza kuwa, Serikali imeendelea kuweka kipaumbele katika ustawi wa wananchi kupitia sekta ya ardhi ili kuhakikisha ardhi inachangia maendeleo yao.
Amesisitiza kuwa, ni wajibu wa kila mwananchi kuhakikisha ardhi inatumika kwa kuzingatia sheria, mipango ya matumizi bora ya ardhi na taratibu zilizowekwa ili kuzuia migogoro.
“Serikali inatambua umuhimu wa ardhi katika maisha na maendeleo ya wananchi. Hivyo, ni jukumu letu sote kuhakikisha ardhi inatumika kwa kuzingatia sheria,” amesema Mhe. Akwilapo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Martin Shigela amewataka wananchi wa vijiji hivyo kufuata maelekezo yaliyotolewa na Serikali na wao kama serikali ya Mkoa itaenda kuhakikisha inatoa maelekezo kwa viongozi wa mitaa na vijiji juu ya uuzaji wa viwanja kiholela alioueleza kuwa unasababisha migogoro.