Habari
WANANCHI WATAKIWA KUJIHAKIKISHIA MIPAKA YA MAENEO WANAYOMILIKI KABLA KUANZA UJENZI
- 17 Oct, 2025

Mkurugenzi wa Maendeleo ya Makazi nchini Bw. Deogratius Kalimenze amewataka wananchi kujiridhisha na uhalali wa mipaka ya maeneo wanayomiliki sambamba na kupata vibali vya ujenzi kutoka halmashauri husika kabla ya kuanza kuyaendeleza ili kuepuka migogoro ya ardhi.
"Ni wajibu wa kila mwananchi kujihakikishia mipaka ya kiwanja chake kabla ya kuanza ujenzi, sambamba na kupata kibali kutoka katika Halmashauri husika" amesema Kalimenze.
Mkurugenzi huyo wa Maendeleo ya Makazi ametoa kauli hiyo tarehe 16 Oktoba 2025 alipofika eneo la kiwanja cha Ndege katika halmashauri ya Mji Nzega mkoani Tabora kwa lengo la kutatua mgogoro wa ardhi ulioripotiwa na Bi. Bertha Temba katika Kliniki ya Ardhi inayoendelea viwanja vya Community Centre.
Katika mgogoro huo, mwananchi wa eneo la Kiwanja cha Ndege katika Halmashauri ya Mji wa Nzega, Bw. Salum Duke, mkazi wa eneo la Kiwanja cha Ndege, alipatiwa ushauri na maelekezo kuhusu marekebisho ya nyumba yake iliyogusa eneo la barabara kwa umbali wa mita tatu.
‘‘Tunapopanga miji tunazingatia upatikanaji wa huduma muhimu kama barabara, mifereji na maeneo ya jamii. Ni muhimu kila mwananchi ajue mipaka ya kiwanja chake kabla ya kujenga na kupata kibali cha ujenzi kutoka Halmashauri husika. Kufanya hivyo kunasaidia kuepuka migogoro na kuboresha mandhari ya miji yetu,” amesema Bw. Kalimenze.
Kwa upande wake, Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Tabora, Bw. Tumaini Gwakisa, amesema ofisi za ardhi zipo wazi kwa wananchi wote, na yeyote ambaye hana uhakika na mipaka yake anapaswa kuwasiliana na wataalamu wa ardhi ili kuonyeshwa mipaka sahihi kabla ya kuendeleza eneo lake.
“Kwa mujibu wa Sheria za Ardhi mwananchi ana wajibu wa kulinda mipaka ya ardhi yake na kuhakikisha anaitumia kulingana na matumizi yaliyopangwa. Hii itapunguza migogoro ya ardhi kwa kiasi kikubwa,” amesema Bw. Gwakisa.
Kliniki ya Ardhi ni sehemu ya jitihada za Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kusogeza huduma za ardhi karibu na wananchi. Hadi kufikia tarehe 16 Oktoba 2025 migogoro 6 kati ya 11 imetatuliwa katika kliniki inayoendelea katika Halmashauri ya Mji Nzega.