Habari
WANANCHI WAPONGEZA HUDUMA ZA ARDHI KATIKA TAMASHA LA UTAMADUNI
- 27 Aug, 2026
Wananchi wameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kushiriki katika Tamasha la Nne la Kitaifa la Utamaduni linalofanyika katika Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro, wakisema ushiriki huo umewawezesha kupata elimu na huduma za ardhi kwa urahisi.
Pongezi hizo zimetolewa na Bw. Kanoni Charles Pita Pangapanga, mkazi wa Manispaa ya Morogoro, baada ya kupokea hati yake katika banda la Wizara ya Ardhi lililopo katika uwanja huo.
Amesema anaiishukuru Serikali na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuboresha huduma za ardhi, akibainisha kuwa wananchi sasa wanapata huduma kwa ufanisi na hati za miliki kutolewa kwa muda mfupi.
Aidha, amesema uwepo wa wataalamu wa ardhi katika tamasha hilo umewarahisishia wananchi kupata majibu ya changamoto zao, pamoja na kuelewa taratibu sahihi za umiliki na matumizi ya ardhi.
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi inaendelea kutumia matamasha na maonesho mbalimbali kusogeza huduma karibu na wananchi, kutoa elimu kuhusu masuala ya ardhi na kuwasaidia kupata huduma moja kwa moja.
Tamasha hilo lilizinduliwa tarehe 26 Agosti 2026 na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mheshimiwa Adamu Malima, ambaye aliwataka Watanzania kuthamini, kulinda na kuendeleza utamaduni wao kwa kuwa ni msingi wa kujenga umoja, uzalendo na mshikamano wa kitaifa.
Amesema tamasha hilo pia ni fursa ya kuendeleza na kuhifadhi utamaduni wa Tanzania, huku Serikali ikiendelea kusogeza huduma mbalimbali karibu na wananchi.