Habari

WANANCHI WAJITOKEZA UZINDUZI KLINIKI YA ARDHI MTWARA

  • 25 Sep, 2026
WANANCHI WAJITOKEZA UZINDUZI KLINIKI YA ARDHI MTWARA

Wananchi Mkoa wa Mtwara wanaendelea kujitokeza kwa wingi kushiriki katika uzinduzi wa Kliniki za ardhi Kidijiti, huku wataalamu wa ardhi wakijipanga kuhakikisha wananchi wanapata huduma za ardhi kwa ufanisi kupitia mfumo huo wa kidijiti.
 

Uzinduzi huo unaofanyika leo tarehe 25 septemba 2026 mkoani Mtwara unaongozwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo, ambaye ni Mgeni Rasmi katika uzinduzi wa huduma za e-Ardhi.
 

Viongozi mbalimbali wa Serikali na Wizara wamewasili Mtwara kushiriki katika tukio hilo muhimu, akiwemo Kamishna wa Ardhi Msaidizi, Idara ya Utawala wa Ardhi, Bi. Hellen Philip, pamoja na Mkurugenzi wa Idara ya TEHAMA Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Fratern Hassan.
 

Uzinduzi huo unafanyika sambamba na utoaji wa huduma za e-Ardhi kwa wananchi, ukiwa sehemu ya jitihada za Serikali za kuimarisha upatikanaji wa huduma za ardhi kwa njia ya kidijiti, kurahisisha huduma na kupunguza ulazima wa wananchi kufuatilia huduma hizo kwa njia za kawaida.


Kliniki ya Ardhi Kidijiti inaendelea kutolewa katika mikoa mbalimbali nchini, ambapo baada ya uzinduzi wa kitaifa, mikoa yote itaendelea kutoa huduma hizo za kidijiti hadi tarehe 3 Oktoba 2026, kwa lengo la kuwafikia wananchi kwa ufanisi zaidi.