Habari

WANANCHI WAHIMIZWA KUTOUPUUZA WITO WA KUITWA SHAURINI KATIKA MABARAZA YA ARDHI

  • 31 Jul, 2026
WANANCHI WAHIMIZWA KUTOUPUUZA WITO WA KUITWA SHAURINI KATIKA MABARAZA YA ARDHI

Wananchi wamehimizwa kutambua umuhimu wa kuitikia wito wa kuitwa shaurini na kuhudhuria vikao vya usikilizwaji wa mashauri ya ardhi kwa wakati, kwani kutofanya hivyo kunaweza kuathiri haki na maslahi yao ya kisheria.

 

Rai hiyo imetolewa na Msajili Msaidizi wa Mabaraza ya Ardhi, Bi. Dorothy Philip, wakati akizungumza katika kipindi cha "Sema Nao" kinachorushwa kupitia ABM FM Radio 91.2 Dodoma.

 

Akizungumza kuhusu mada isemayo "Wito wa Kuitwa Shaurini: Maana, Wajibu wa Wadaawa na Madhara ya Kupuuza Wito," Bi. Dorothy alisema kuwa wito wa kuitwa shaurini ni taarifa rasmi inayomtaka mhusika kufika mbele ya Baraza la Ardhi kwa tarehe, muda na mahali vilivyobainishwa ili kushiriki katika usikilizwaji wa shauri.

 

Alieleza kuwa wadaawa wana wajibu wa kuitikia wito huo, kuhudhuria vikao vya usikilizwaji wa mashauri na kuwasilisha hoja au ushahidi wao kwa mujibu wa sheria. Aliongeza kuwa kupuuza wito bila sababu za msingi kunaweza kufanya shauri kuendelea na kuamuliwa bila ushiriki wa mhusika.

 

Aidha, aliwataka wananchi kuhifadhi nyaraka zote wanazopewa na Mabaraza ya Ardhi, kuzingatia tarehe za usikilizwaji wa mashauri na kufuata taratibu za kisheria ili kulinda haki zao.

 

Mabaraza ya Ardhi yanaendelea kutoa elimu kwa wananchi kupitia vipindi mbalimbali vya redio, televisheni na mitandao ya kijamii kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu sheria, taratibu za usikilizwaji wa mashauri ya ardhi, pamoja na haki na wajibu wa wananchi katika kupata na kutafuta haki kwa mujibu wa sheria.