Habari
WANANCHI WAHIMIZWA KUCHANGAMKIA FURSA ZA KUPATA HATI ZA ARDHI
- 31 Aug, 2026
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Kaspar Mmuya, amewataka wananchi ambao maeneo yao yamepimwa na kutambuliwa kisheria kuanza mara moja mchakato wa kuomba hati za umiliki wa ardhi ili kuimarisha usalama wa milki zao na kupunguza migogoro ya ardhi.
Mhe. Mmuya amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua za kudhibiti urasimu na mianya ya rushwa katika utoaji wa huduma za ardhi, huku akiwataka wananchi kutumia fursa zilizopo kisheria kupata hati za maeneo yao.
Ametoa kauli hiyo, Agosti 29, 2026, alipotembelea banda la Kliniki ya Ardhi la Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi katika kilele cha Tamasha la Nne la Kitaifa la Utamaduni mkoani Morogoro.
Katika hatua nyingine, Mhe. Mmuya amewapongeza watumishi wa sekta ya ardhi kwa kuendelea kujitoa kwa dhati kuwahuduma wananchi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za taaluma, akisisitiza umuhimu wa kuongeza kasi ya utoaji wa huduma bila kuvunja misingi ya sheria.
Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Morogoro, Idrisa Kayera, amesema hadi kufikia tamati ya tamasha hilo, Kliniki ya Ardhi Morogoro imefanikiwa kutoa takribani hati 800 za kimila kwa wananchi, huku idadi ya wanawake waliopata hati ikiongezeka, hatua inayokwenda sambamba na utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995 toleo la mwaka 2023 kuhusu haki sawa za umiliki wa ardhi.