Habari
WANANCHI MATONGO NA NYANGOTO KUELIMISHWA KUHUSU UTHAMINI WA FIDIA NORTH MARA
- 27 Aug, 2026
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kupitia wataalamu kutoka Ofisi ya Mthamini Mkuu wa Serikali, imefanya kikao na Kampuni ya Barrick North Mara Gold Mine pamoja na viongozi wa Vijiji vya Matongo na Nyangoto, kwa lengo la kujadili maandalizi ya utoaji elimu kwa wananchi kuhusu zoezi la uthamini wa fidia linalohusishwa na upanuzi wa shughuli za Mgodi wa North Mara.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho, Diwani wa Kata ya Matongo, Mhe. Godfrey Mwita, amewataka viongozi wa Vijiji vya Matongo na Nyangoto kushirikiana kwa karibu na wataalamu pamoja na wadau wote wanaohusika katika mchakato huo, akieleza kuwa wananchi wa maeneo hayo wanatarajiwa kuguswa na upanuzi wa shughuli za mgodi.
Kwa upande wake, Meneja wa Mahusiano wa Kampuni ya Barrick, Bw. Francis Uhadi, amesema kampuni hiyo iko tayari kuanza mchakato huo kwa haraka, huku akisisitiza dhamira ya kampuni kuhakikisha haki na maslahi ya wananchi yanazingatiwa na kulindwa kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi.
Akifafanua hatua zinazofuata, Mthamini Kiongozi kutoka Ofisi ya Mthamini Mkuu wa Serikali, FRV. Baraka D. Mollel, amesema kikao hicho ni sehemu ya hatua muhimu kuelekea kuanza mchakato wa uthamini, baada ya hatua za awali zilizofanyika kwa kushirikisha Wizara ya Madini, ikiwemo tafiti na maandalizi mbalimbali.
Amesema hatua hizo zinalenga kuhakikisha zoezi la uthamini linafanyika kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu, pamoja na kuwezesha wananchi kupata taarifa sahihi kuhusu mchakato huo.
Naye Mtunzaji wa Bwawa la Mgodi, Bw. Majuto Kipande, ameeleza kuwa, tafiti za awali zilizofanyika wakati wa uanzishwaji wa mgodi zilionesha kuwa shughuli za uzalishaji zingefikia ukomo mwaka 2027. Hata hivyo, amesema tafiti zinazoendelea hivi sasa zinaonesha uwezekano wa uzalishaji kuendelea hadi kati ya mwaka 2031 na 2040.
Kwa mujibu wa Kipande, hali hiyo imeongeza umuhimu wa upanuzi wa bwawa la kutunza mabaki ya uchenjuaji wa dhahabu kutokana na bwawa linalotumika sasa kutaraji kufikia ukomo wa matumizi mwaka 2031.
Ameongeza kuwa, ujenzi wa bwawa jipya la kutunza mabaki ya uchenjuaji wa dhahabu unapaswa kukamilika kabla ya mwaka 2031, ili kuwezesha shughuli za mgodi kuendelea bila kuathiriwa na ukomo wa uwezo wa bwawa linalotumika sasa.
Mchakato wa uthamini unalenga kuhakikisha wananchi watakaoguswa na eneo la upanuzi wanapatiwa elimu na taarifa sahihi kuhusu hatua zinazochukuliwa, huku zoezi la uthamini wa fidia likitekelezwa kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za nchi.