Habari
WANANCHI KIJIJI CHA UBEMBE WATAKIWA KUHESHIMU MIPANGO YA MATUMIZI YA ARDHI
- 18 Mar, 2026
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imewataka wananchi wa kijiji cha Ubembe wilaya ya Muheza mkoa wa Tanga kuheshimu mipango ya Matumizi ya Ardhi iliyowekwa ili kuepuka migogoro ya ardhi.
Aidha, Kamati hiyo imetoa maelekezo wananchi wa kijiji hicho cha Ubembe kupatiwa hati milki za ardhi ndani ya siku 60.
Akizungumza wakati wa mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Ubembe Wilaya Muheza mkoani Tanga, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Mhe. Timotheo Mzava amesema kufanya mipango ya matumizi ya ardhi ni jambo moja, kuiheshimu na kuisimamia ni jambo jingine.
“Ni maombi na wito wetu kwenu, kazi hii nzuri iliyofanyika na kutumia fedha za walipa kodi wa nchi hii mkiwemo ninyi wana Ubembe, ili iwe na maana na faida, ni wajibu wenu ninyi kwenda kuuheshimu mpango huu mliojiwekea wenyewe.”
“Hatutarajii kusikia baada ya mpango huu kuna mkulima anakwenda kulima sehemu ya kuchungia, mfugaji anakwenda kuchunga kwenye maeneo ya kilimo na sehemu nyingine za mpango. Kila mmoja akaishi na kufanya majukumu yake kulingana na mpango wa matumizi ya ardhi tulioutengeneza wenyewe na tuliokubaliana” amesema Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Mzava.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Kaspar Mmuya amesema, Wizara yake imeyapokea maelekezo ya Kamati na imeiahakikishia kuwa ndani ya siku 60 kazi kutoa hati kwa wananchi hao wa Kijiji cha Ubembe itafanyika.
Utekelezaji wa Mradi wa Upangaji wa Matumizi ya Ardhi (Namba 4951) katika Halmashauri ya Wilaya ya Muheza umechangia kuwa na vijiji 357 sawa na asilimia 46.79 vilivyo na Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya vijiji kati ya vijiji 763 vilivyopo katika Halmashauri za Wilaya nane zilizopo Mkoa wa Tanga.
Katika Halmashauri ya Wilaya ya Muheza utekelezaji wa mradi huu umefanyika kwa kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji nane vya Mindu, Lunguza, Mkuzi, Mgome, Mpapayu, Ubembe, Misongeni na Enzi.
Idadi hiyo inakamilisha kuwa na jumla ya vijiji 46 sawa na asilimia 36.51 vyenye mipango ya Matumizi ya Ardhi kati ya vijiji 126 vilivyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Muheza.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Muheza Mhe. Ayubu Sebabili, amesema, watasimamia na kutoa ushirikiano wa dhati kuhakikisha mpango huo wa matumizi bora ya ardhi katika Kijiji cha ubembe na vijiji vingine ambavyo vinatekeleza mradi huo unafanyika na kutekelezwa kwa mujibu wa mpango.