Habari
WANANCHI HALE KUNUFAIKA NA VIWANJA 3,104 VYA MPANGO WA KKK MAKINYUMBI
- 19 Nov, 2026
Wananchi wa Kata ya Hale, Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga, wanatarajia kunufaika na viwanja 3,104 vilivyozalishwa kupitia Mpango wa Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi (KKK), unaotekelezwa katika eneo la Shamba la Makinyumbi lenye ukubwa wa ekari 1,892.
Mpango huo ni sehemu ya juhudi za Serikali kuhakikisha ardhi inatumika kwa tija kupitia upangaji, upimaji na umilikishwaji unaozingatia sheria na taratibu, hatua inayolenga kuwawezesha wananchi kupata maeneo yenye uhakika wa kisheria na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Kwa mujibu wa mpango wa uendelezaji wa ardhi katika eneo hilo, jumla ya ekari 5,000 zimetengwa kwa matumizi mbalimbali yakiwemo kilimo, makazi, huduma za jamii, miundombinu, ardhi ya akiba, uwekezaji na uchimbaji madini, pamoja na hifadhi ya mlima na vyanzo vya maji.
Aidha, ekari 4,220 zimetengwa katika vijiji vya Makinyumbi Station na Miembeni, na kufanya jumla ya eneo lote lililojumuishwa katika mpango huo wa uendelezaji kufikia ekari 9,220.
Akielezea utekelezaji wa zoezi hilo, Kiongozi wa Timu ya Wataalamu kutoka Wizara ya Ardhi ambaye pia ni Afisa Ardhi Mwandamizi, Bw. David Emanuel Malisa, amesema kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha ardhi inapangwa na kupimwa kwa kuzingatia sheria na taratibu ili wananchi waweze kupata maeneo yenye uhakika wa umiliki kisheria.
"Awali zoezi hili lilikuwa likisimamiwa na Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Tanga kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe, lakini baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi na Maliasili na Utalii kutembelea eneo hilo, ilielekeza usimamizi wa utekelezaji wake ufanywe na Wizara ya Ardhi". Amesema Bw. Malisa
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Mwakinyumbi Miembeni, Bw. Idd Sandari Saidi, amesema uongozi wa kijiji umepokea kwa matumaini utekelezaji wa mpango huo kutokana na manufaa yake kwa wananchi, hususan katika kupata uhakika wa maeneo yao na kuongeza fursa za maendeleo.
Amesema, utekelezaji wa zoezi hilo umeongeza matumaini na amani miongoni mwa wananchi kwa kuwa utaratibu wa kutambua, kupanga na kupima maeneo unaweka msingi wa umiliki salama na matumizi bora ya ardhi.
Eneo la mradi huo awali lilikuwa likimilikiwa na Kampuni ya M/S Makinyumbi, iliyopewa ardhi hiyo mwaka 1989 kwa ajili ya uwekezaji katika kilimo cha mkonge. Hata hivyo, kampuni hiyo ilishindwa kutekeleza masharti ya umilikishwaji, ikiwemo kuliendeleza eneo hilo kama ilivyokuwa imekusudiwa, hali iliyosababisha milki hiyo kubatilishwa mwaka 2023 na ardhi kurejea serikalini.
Septemba 21, 2026, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo, akiambatana na Mbunge wa Jimbo la Korogwe Vijijini, Mhe. Timotheo Mzava, alizindua rasmi Mpango wa Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi (KKK) katika eneo la Shamba la Makinyumbi.
Wakati wa uzinduzi huo, Waziri Akwilapo aliwataka wananchi wanaoishi katika eneo hilo kushirikiana na wataalamu wanaotekeleza zoezi hilo ili kuhakikisha linakamilika ndani ya muda uliopangwa na kuwawezesha kunufaika na mpango huo.