Habari
WANANCHI CHEMBA KUNUFAIKA NA KLINIKI YA ARDHI
- 08 Oct, 2026
Mkoa wa Dodoma umeendelea kutekeleza Kliniki za Ardhi katika maeneo mbalimbali kwa lengo la kusogeza huduma za ardhi karibu na wananchi, ambapo safari hii kliniki hiyo inafanyika Wilayani Chemba kwa siku tano.
Kliniki hiyo iliyoanza Oktoba 5, 2026 katika Ofisi za Ardhi Wilaya ya Chemba, inalenga kutoa elimu na huduma mbalimbali za ardhi kwa wananchi, ikiwemo elimu kuhusu ulipaji wa kodi ya pango la ardhi.
Akizungumza kuhusu kliniki hiyo, Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Dodoma, Bi. Happiness Mtutwa, amesema Serikali kupitia kliniki hiyo inalenga kuhakikisha wananchi wanapata huduma za ardhi kwa urahisi.
Bi. Mtutwa amewataka wananchi wa Chemba kutumia fursa hiyo kufika katika kliniki hiyo ili kupata elimu na huduma zinazohusiana na ardhi, pamoja na kufuatilia masuala yao ya umiliki wa ardhi.
Kliniki hiyo inatarajiwa kuhitimishwa Oktoba 9, 2026 ikiwa ni sehemu ya jitihada za Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuendelea kusogeza huduma za ardhi karibu na wananchi na kuhakikisha wanapata huduma kwa wakati.