Habari
WANANCHI 324 NGEA WAKABIDHIWA HATI ZA KIMILA KUIMARISHA UMILIKI WA ARDHI NA UHIFADHI MAZINGIRA
- 31 Mar, 2026
Wananchi 324 wa kijiji cha Ngea, wilayani Kilwa mkoani Lindi, wamekabidhiwa hati za kimila kupitia Mradi wa Pamoja Tuhifadhi Bahari, hatua inayolenga kuwawezesha kumiliki ardhi kisheria pamoja na kushiriki kikamilifu katika uhifadhi wa mazingira ya ukanda wa pwani.
Mradi huo unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya mashirika ya uhifadhi mazingira WWF , IUCN, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, huku ukifadhiliwa na Umoja wa Jumuiya ya Ulaya (EU). Ukiwa na dhima ya kuimarisha usalama wa umiliki wa ardhi kwa wananchi huku ukihamasisha matumizi endelevu ya rasilimali za mazingira.
Hafla ya kukabidhi hati hizo imefanyika leo tarehe 27 Machi, 2026 katika Ofisi ya Kijiji cha Ngea, ambapo mgeni rasmi alikuwa Kamishna wa Ardhi Msaidizi wa Mkoa wa Lindi, Bw. Geofrey Mugisha. Katika hafla hiyo, Mugisha alikabidhi hati kwa wananchi waliokamilisha taratibu zote za umiliki wa ardhi.
Akizungumza katika tukio hilo, Bw. Mugisha alisisitiza umuhimu wa kuzitunza hati hizo, akieleza kuwa nyaraka hizo zitasaidia kuimarisha usalama wa umiliki wa ardhi, kuongeza thamani ya ardhi pamoja na kuchochea utunzaji bora wa mazingira.
Aidha, aliwataka wananchi kuendelea kuheshimu mipango ya matumizi ya ardhi iliyopo ili kuepusha migogoro na kulinda mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Kwa upande wake, Meneja wa Mradi wa Pamoja Tuhifadhi Bahari Yetu kutoka katika Shirika la Uhifadhi mazingira Duniani (WWF), Bi. Hania Mkogas, alisema mradi huo hauishii tu katika ugawaji wa hati bali pia unajenga uwezo kwa wananchi katika uhifadhi wa mazingira na usimamizi bora wa ardhi.