Habari

WANAMICHEZO ARDHI SPORTS WATAKIWA KUZINGATIA NIDHAMU, KUIPIGANIA WIZARA SHIMIWI

  • 21 Sep, 2026
WANAMICHEZO ARDHI SPORTS WATAKIWA KUZINGATIA NIDHAMU, KUIPIGANIA WIZARA SHIMIWI

Wanamichezo wanaoshiriki Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara, Idara na Taasisi za Serikali nchini (SHIMIWI) 2026 inayotarajiwa kufanyika Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro kuzingatia nidhamu, uwajibikaji na maadili ya Utumishi wa Umma kipindi chote cha mashindano.

 

Hayo yamesemwa na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bi. Salome Kessy Septemba 18, 2026 jijini Dodoma wakati akiwaanga wanamichezo wa Wizara wanaoshiriki michuano hiyo.

 

Mafanikio katika michezo hayawezi kutenganishwa na nidhamu, kila mmoja abebe taswira ya Wizara. Tunzeni utimamu wa miili yenu, zingatieni ushauri wa madaktari, kula vizuri na kupumzika kwa wakati badala ya kutumia muda wa mapumziko kuzurura" amesema Bi. Salome.

 

Aidha, amewataka viongozi na walimu wa timu kuhakikisha kila mchezaji anawajibika ipasavyo huko wakibeba vema taswira ya Wizara na kusisitiza kuwa vitendo vya utovu wa nidhamu havitavumiliwa na hatua stahiki zichukuliwe kwa watakaokiuka taratibu za timu na maadili ya Utumishi wa Umma.

 

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Klabu ya Michezo ya Wizara ya Ardhi Bw. Swagile Msananga ameishukuru Wizara kwa kuweka mazingira mazuri ya maandalizi ya timu, ambapo wanamichezo wamefanya mazoezi kwa zaidi ya mwezi mmoja sambamba na kushiriki mabonanza matatu pamoja na michezo ya majaribio, hatua aliyoieleza kuwa inaenda kusaidia timu kupata ushindani na kujiimarisha kuelekea SHIMIWI.

 

Ameeleza kuwa katika mabonanza hayo, timu ya Kuvuta Kamba Wanawake na timu ya Mpira wa Miguu zilifanikiwa kutwaa vikombe viwili, jambo alilolitaja kuwa ni ishara ya maandalizi mazuri na kusisitiza kuwa, wanamichezo hao wanaenda kutumia uzoefu huo kuongeza juhudi katika mashindano hayo.

 

Jumla ya wanamichezo 96 wanaiwakilisha Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi katika michezo ya mpira wa miguu, mpira wa pete, kuvuta kamba, riadha, karata, bao, kurusha tufe, darts na draft.

 

Michuano hiyo inatarajiwa kufanyika mkoani Kilimanjaro kuanzia Septemba 20 na kuhitimishwa Oktoba 7, 2026 ikiongozwa na Kaulimbiu inayohimiza utayari wa Watumishi wa Umma kuelekea michuano ya Afrika (AFCON) 2027 inayoandaliwa na Tanzania, Kenya na Uganda.