Habari
WAKURUGENZI WA KAMPUNI ZA MIPANGOMIJI WANOLEWA, WATAKIWA KUONGOZA MAGEUZI YA SEKTA YA MIPANGOMIJI
- 16 Apr, 2026
Wakurugenzi wa kampuni za mipangomiji zilizosajiliwa Tanzania Bara wametakiwa kuongoza mageuzi makubwa yatakayochochea ukuaji wa sekta hiyo na kuhakikisha miji inapangwa kwa viwango vinavyokidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Makazi kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, TP. Deogratius Kalimenze, wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wakurugenzi wa kampuni za mipangomiji yaliyoandaliwa na Bodi ya Usajili wa Wataalamu wa Mipangomiji (TPRB) jijini Dar es Salaam.
TP. Kalimenze amesisitiza umuhimu wa kuzingatia maadili ya taaluma, akiwataka wataalamu hao kushirikiana kwa karibu na Serikali katika kubaini na kudhibiti vitendo vya watu wanaofanya kazi za mipangomiji bila kufuata taratibu, ikiwemo kutosajiliwa na TPRB.
Kwa upande wake, Kaimu Msajili wa TPRB, TP. Martha Mkupasi, amesema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo wakurugenzi hao kwa kuwapatia jukwaa la kujadili changamoto wanazokutana nazo, kubaini mbinu za kuzitatua pamoja na kubadilishana uzoefu wa kitaaluma.
Ameeleza kuwa jukwaa hilo ni muhimu katika kuimarisha taaluma ya mipangomiji, huku likichochea utekelezaji wa sheria, kanuni na taratibu ili kufanikisha ujenzi wa miji endelevu, jumuishi na inayokidhi viwango vya kitaifa na kimataifa.
Wakizungumza baada ya mafunzo hayo, baadhi ya wakurugenzi wa kampuni za mipangomiji wameishukuru TPRB kwa kuandaa mafunzo hayo, wakieleza kuwa yamekuwa chachu ya mabadiliko chanya katika uendeshaji na utoaji wa huduma ndani ya kampuni zao.